Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezindua barabara ya Tunduma - Laela - Sumbawanga yenye urefu wa kilometa 223.2 ambayo ni sehemu ya barabara kuu katika ushoroba wa magharibi unaonzia Tunduma - Mpanda - Kigoma - Nyakanazi wenye urefu wa kilometa 1,286.
Ujenzi wa barabara hiyo umegharimu shilingi Bilioni 373 na Milioni 949 kwa ufadhili wa mfuko wa changamoto za milenia (MCC) na kukamilika kwake kumesaidia kuinua shughuli za kiuchumi katika ukanda wa nyanda za juu kusini na ukanda wa magharibi, na pia kumeunganisha usafiri kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa barabara hiyo zilizofanyika katika Mji Mdogo wa Laela Wilayani Sumbawanga, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mikoa yote inayonufaika na barabara hiyo na amewahakikishia kuwa Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha barabaa kuu zote za ukanda wa magharibi zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Ameishukuru Marekani kupitia MCC kwa ufadhili wa mradi huo, Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa mradi huo kutekelezwa katika kipindi chake na ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo, na pia amewataka wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kutunza miundombinu yake kwa kutochimba mchanga kando ya barabara na madaraja, kutomwaga mafuta barabarani na kutoiba alama za barabarani.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kuchukizwa na taarifa za kuchomwa moto mitambo ya umeme jua ya mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Laela uliogharimu shilingi Bilioni 1.7 na ameagiza waliohusika kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha, baada ya kupokea malalamiko dhidi ya mkandarasi Fally Enterprises Ltd aliyepatiwa zabuni ya kujenga mradi huo pamoja na miradi mingine ambayo inadaiwa kutofanya kazi kama ilivyotarajiwa licha ya fedha zake kulipwa , Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 7 kwa vyombo vya dola kumkamata, kuchunguza na kumfikisha katika vyombo vya sheria, na pia ameagiza Wizara ya Maji kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wote wa wizara waliohusika kumpa zabuni mkandarasi huyo.
Chanzo: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.