Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 11 Juni, 2020 alizindua majengo ya Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, na aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Makao Makuu Dodoma na kukabidhi pikipiki 448 za Maafisa Tarafa hapa nchini.
Sherehe za uzinduzi wa jengo la TARURA, uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kilometa 51.2 za barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kukabidhi pikipiki 448 za Maafisa Tarafa, zilifanyika katika Mji wa Serikali Mtumba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.
Jengo la Makao Makuu ya TARURA ambalo ni la ghorafa 2, mita za mraba 1,961, ofisi 34 na ukumbi wa mikutano, limejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 969 kwa kutumia utaratibu wa 'Force Account' ambao umesaidia kuokoa fedha nyingi, badala ya utaratibu wa kutumia mkandarasi ambao ungegharimu zaidi shi shilingi Bilioni 7.
Ujenzi wa Barabara za lami ngumu ya Mji wa Serikali zenye urefu wa kilometa 51.2 ambao umeanza tarehe 01 Februari, 2020, unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Julai, 2021 kwa gharama ya shilingi Bilioni 89.232 ambapo kilometa 11.2 zitakukwa na njia 4 na kilometa 28.8 zitakuwa na njia mbili.
Pikipiki 448 zilizonunuliwa kwa ajili ya Maafisa Tarafa zimegharimu shilini Bilioni 1 na kununuliwa kwake kutafanya Maafisa Tarafa wote hapa nchini kuwa na pikipiki kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe, Magufuli aliipongeza TARURA kwa kujenga ofisi ya makao yake makuu kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha na kwa kuanza ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali, na pia amezipongeza wizara, idara na taasisi zingine za Serikali zilizojenga ofisi zake katika Mji wa Serikali. Alielezea kuridhishwa kwake na maendeleo makubwa ya Mji wa Serikali na Jiji zima la Dodoma.
Hata hizo aliitaka TARURA kutojenga ofisi zake Wilayani na Mikoani, badala yake watumie majengo ya Serikali yaliyopo, na ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha jengo lake la makao makuu linalojengwa Dodoma linakamilika ndani ya mwaka huu, badala ya kutumia majengo yasiyo yake.
Mhe. Rais alisema licha ya kwamba wapo ambao hawakuamini kuwa Serikali inaweza kuhamia Dodoma, jambo hilo limewezekana ambapo watumishi wa umma 13,361 wamehamia Dodoma, viongozi wakuu wote wakiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamehamia Dodoma. Alilipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha sheria ambayo inatambua rasmi kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi.
Aidha, alibainisha kuwa sambamba na mafanikia hayo, Serikali inachukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za kijamii katika Jiji la Dodoma ikiwemo kujenga hospitali, kujenga kilometa 110 za barabara ya mzunguko, kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato, soko, kituo cha mabasi na kuimarisha barabara za ndani ya Jiji.
Vile vile, Mhe. Rais alilishukuru Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kutoa msamaha wa Dola za Marekani Milioni 14 (sawa na shilingi Bilioni 31.934) kwa Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa Corona.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mitambo itakayotumika kwenye ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba zenye jumla ya kilometa 51.2 tarehe 11 Juni, 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seif kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara za lami kwenye Mji wa Serikali Mtumba zenye urefu wa kilometa 51.2 Jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo wakivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa barabara za lami zenye jumla ya km 51.2 katika Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Juni, 2020.
Rais Mhe. Dkt. John Magufuli akizungumza na wafanyakazi mbalimbali wa Serikali kabla ya kufungua Jengo la Ofsisi za makao makuu ya TARURA mjini Dodoma tarehe 11 Juni, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.