Yaliyojiri wakati wa mahojiano ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, na Kaimu Meneja Mawasiliano wa TANESCO, Leila Muhaji, kwenye vituo vya radio Imaan na Abood, Morogoro kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa umeme Rufiji.
#Kwanza kabisa tunawahakikishia Watanzania popote walipo kwamba Serikali yao ipo kazini katika kila nyanja;
#Kubwa kuliko yote wiki hii ni ya kihistoria, tunakwenda kuzindua rasmi ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Mto Rufiji;
#Tunakwenda kuzindua rasmi safari ya miaka mitatu ya ujenzi huo ikiwa ni baada ya miaka 39 ya kushindwa kuutekeleza mradi kufuatia utafiti wa awali wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza kuonesha gharama zilikuwa kubwa sana;
#Mradi huu ilikuwa ndoto ya Baba wa Taifa pamoja na ndoto nyingine ikiwemo ile ya Makao Makuu kuhamia Dodoma na ujenzi wa Daraja la Sibiti, kwa hiyo mengine tumeyatimiza, mradi huu nao tunatekeleza ndoto za Baba wa Taifa;
#Mradi huu wa Megawati 2,115 utaondoa matatizo ya uhakika wa nishati ya umeme ambao utakuwa ni kichocheo cha Tanzania ya Viwanda;
#Huu mradi kwa faida zake kwa nchi ilikuwa lazima siku moja utekelezwe, hata kama Awamu zote na hii ya sasa zisingeutekeleza ipo siku bado ungetekelezwa tu;
#Mradi huu licha ya faida zake kwa uchuni wa viwanda pia utasaidia kupunguza gharama za umeme kwa sababu uzalishaji wa umeme wa maji ni rahisi kuliko vyanzo vingine vyote;
Kwa mfano, wakati Unit 1 ya umeme wa maji ni shilingi 36; Uniti 1 ya Umeme wa Joto ardhi ni Shilingi 147, Uniti 1 ya umeme wa Mafuta ni Shilingi 546, Uniti 1 ya Umeme wa Makaa ya mawe ni Shilingi 118, Umeme wa Upepo ni Shilingi 103 kwa Uniti 1 na umeme wa jua ni Shilingi 103.5 kwa Uniti 1;
#Kuhusu madai kwamba kuna athari za mazingira, ifahamike kuwa hakuna mradi duniani usiogusa mazingira, kila mradi uliotekelezwa hata Ulaya na kwingineko umegusa mazingira, hoja kubwa ni kuhakikisha athari za mazingira haziwi kubwa au hazizidi faida ya mradi husika kuwepo;
#Katika mradi huu hakuna athari zinazozidi manufaa ya mradi kwa nchi na watu wake, lakini pia wanaozungumzia uhifadhi wajue Mbuga ya Selous ina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000 na eneo litakalotumika kwa ajili ya mradi na mambo yote ya mradi ikiwemo bwawa havitazidi asilimia 4 ya eneo lote la Selous kwa hiyo uhifadhi wa wanyama na miti utaendelea kuwepo;
#Kwa hiyo wanaoupinga mradi huu tuwasamehe tu, lakini tujue kwamba wapingaji walikuwepo tangu enzi za manabii na hata tusingeutekeleza mradi huu wapo ambao wangehoji kwa nini hatujauanza?
#Serikali inaendelea pia kuhakikisha maandalizi muhimu ya mradi yamekamilika ikiwemo kuingiza megawati 30 za umeme unaohitajika kusaidia mradi kutekelezwa;
#Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Tanesco yenyewe zimeshiriki katika maandalizi ya mradi na sasa mkandarasi amekabidhiwa na anaanza kazi;
#Mradi huu ipo siku wanaopinga wataelewa faida zake; bahati nzuri wanaopinga ndio hao hao siku ukikamilisha jambo wanakuwa mbele kunufaika. Kuna mtu alipinga sana ndege, mara anasema sio mpya mara nini, siku moja tukamuona amepanda ndege hizo hizo, kwa hiyo ndio maisha.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi (kulia) akitoa ufafanuzi juu ya maandalizi ya uzinduzi wa Mradi mkubwa ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji kwenye Mto Rufiji. Kushoto kwake ni Kaimu Meneja Mawasiliano wa TANESCO, Leila Muhaji.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa TANESCO, Leila Muhaji akifafanua jambo wakati akitoa ufafanuzi wa ushiriki wa TANESCO kwenye maandalizi ya Uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Mradi wa kufua umeme wa maji kwenye Mto Rufiji.
Chanzo: Idara ya Habari - MAELEZO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.