Na. Rahma Abdallah, MPUNGUZI
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri amewataka washiriki wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwa muda wote wa mafunzo na kuzingatia yote watakayo fundishwa ili kuwa kuwa askari mahili.
Hayo aliyasema wakati akifungua mafunzo ya 17 ya Jeshi la Akiba Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa michezo wa Shule ya Sekondari Mpungunzi iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa wakufunzi wa mafunzo hayo wanauzoefu mkubwa utakaowasaidia kuimarika katika kozi mbalimbali za jeshi la akiba. “Niwaase mfuate maelekezo, mfuate mafunzo yote ya medani, mafunzo ya kitendaji, pia kuwa na nidhamu wakati wote wa mafunzo. Msingi mkubwa wa kazi za jeshi ni nidhamu. Huwezi kuwa askari kama huna nidhamu. Kwahiyo, mtapimwa viwango vyenu vya nidhamu” alisema Alhaj Shekimweri.
Pia aliongeza kwa kusema “tafsiri ya kwanza ya nidhamu ni kuheshimiana ninyi kwa ninyi, kuwaheshimu viongozi wenu wa kambi, kuwaheshimu viongozi wanaokuja kuwatembelea na kuwatia nguvu huku mkitambua kuwa yote mnayoyafanya ni chini ya mwamvuli wa jeshi la ulinzi na usalama wa nchi yetu”.
Sanjari na hayo aliwasisitiza kujitokeza na kushiriki katika uboreshaji wa taarifa kwenye daftari la mpira kura pamoja na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2024. “Hakikisheni mnahuisha taarifa zenu na kwa wale ambao walikuwa na umri mdogo katika uchaguzi uliopita na sasa wamefikia umri wa kushiriki mkajiandikishe. Ukiona una sifa za kuwa kiongozi, chukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali na wakati ukifika shiriki kumpigia kura kiongozi atakayekufaa” Alhaj Shekimweri alisisitiza.
Alihitimisha kwa kuwapongeza washiriki wa mafunzo kwa utayari wao na uzalendo na kuwatakia heri katika muda wote wa mafunzo. Aidha, aliwataka wakufunzi wa mafunzo hayo kuwaandaa kikamilifu washiriki hao ili wawe raia wema kwa nchi yao.
Akiwasilisha taarifa ya mafunzo hayo, SSGT. Lusajo Mwakanyamale, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Dodoma alisema kuwa washiriki wa mafunzo hayo wametoka tarafa ya Dodoma mjiji pamoja na Zuzu. Alisema baadhi yao ni walinzi kutoka makampuni binafsi na wengine ni kutoka kwenye mitaa wanayoishi kwa mujibu wa sheria. “Afande mgeni rasmi napenda kukuhakikishia kuwa mafunzo haya yatafikia viwango vinavyokubalika na jeshi la akiba na watakuwa tayari kulitumikia taifa. Mafunzo haya yatafanyika kwa majuma 18 (miezi 4)” alisema SSGT. Mwakanyamale.
Mafunzo ya Jeshi la Akiba Wilaya ya Dodoma ni mafunzo ya awamu ya 17 yakilenga kuwajengea washiriki utimamu wa mwili, ukakamavu, ujasiri na uzalendo kwa taifa lao kupitia masomo mbalimbali ikiwa ni pamoja na usalama wa raia, huduma ya kwanza, ramani, zimamoto, uhamiaji na elimu ya kupambana na rushwa, alisema SSGT. Mwakanyamale.
Kwa upande wake Lameck Mashaka, Mshiriki wa mafunzo hayo alisema kuwa uzalendo kwa nchi ndio msukumo uliomfanya kujitokeza na kupata mafunzo hayo. Aliahidi kuzingatia mafunzo hayo na kuyafanyia kazi mara baada ya kuhitimu. “Nashukuru kwa kupatiwa nafasi hii ya ushiriki kwenye haya mafunzo na imani yangu kubwa nitaimarika na kwenda kuitumikia nchi yangu kwa uzalendo” alisema Mashaka.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.