WAKAZI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kupanda angalau miti mitano katika makazi yao kwa lengo la kuhifadhi mazingira na utekelezaji wa kampeni ya Kijanisha Dodoma.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alipoongoza kamati ya maandalizi ya siku ya wanawake duniani, Jiji la Dodoma kupanda miti katika shule ya msingi Vikonje jijini hapa.
Nabalang’anya alisema kuwa, zoezi la upandaji miti katika shule hiyo ni maalum kuunga mkono dhamira ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ya kukijanisha Dodoma.
“Changamoto iliyopo Dodoma, ni kwenye makazi yetu hatupandi miti. Kwa hiyo, iwe mwanzo leo, tunapopanda miti katika ngazi ya taasisi, tupande miti kwenye makazi yetu pia. Mtu ukikosa miti mitano nyumbani kwako utakuwa na tatizo” alisema Nabalang’anya kwa masikitiko makubwa.
Alisema kuwa miti inapatikana Halmashauri ya Jiji la Dodoma bure. “Hivyo, nawaambiwa wazi kwa sababu halmashauri yenyewe inatekeleza kwa vitendo agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais. Hivyo, tunaamini miti hii inayopandwa ikitunzwa vizuri, baada ya miaka miwili Dodoma itakuwa ya kijani kuliko hata yale maeneo mengine tuliyozoea kuyaona ya kijani” alisema Nabalang’anya kwa uhakika.
Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje alipongeza uamuzi wa zoezi la upandaji miti kufanyika katika kata yake. “Niahidi kwa niaba ya walimu na wakazi wa Mtumba, miti hii iliyopandwa leo tutaitunza hadi istawi na kukua. Miti hii imekuja kwa fedha za serikali, hivyo, tunawajibu wa kuitunza vizuri ili thamani ya fedha ya serikali ionekane” alisema Maboje.
Aidha, alitoa wito kwa uongozi wa halmashauri kupeleka matukio na shughuli mbalimbali katika kata hiyo yenye mji wa serikali na kuiita ni kata ya kimkakati.
Nae Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Vikonje, Beatrice Chidumizi alisema kuwa suala la uhifadhi na uboreshaji wa mazingira ni la kijamii. “Sisi kama taasisi, kwenye suala la kuboresha na kuhifadhi mazingira ya shule, tunawatumia walimu na wanafunzi. Wapo walimu wazoefu na wabunifu katika kuweka mandhari vizuri. Tunatumia klabu za mazingira hapa shule na kuongozwa na walimu katika kupendezesha mandhari. Kwa sababu na mimi ni mwanamke, wanawake ndiyo chanzo cha usafi wa mazingira hata nyumbani. Nyumba isipokuwa na mwanamke haiwezi kuwa safi. Ndiyo maana utaona mazingira ya hapa yanavutia, wanawake ndiyo watu wanaopenda sana mazingira” alisema Mwl. Chidumizi.
Akiongelea zoezi la upandaji miti katika shule yake, alilitaja kuwa zoezi hilo ni heshika kubwa kwa shule yake. “Kwa siku ya leo, tunapoelekea kwenye kilele cha siku ya wanawake duniani, mazingira yetu yataweza kuboreka na kuwa mazuri zaidi. Tumefurahi zoezi hili kuwa katika Kata ya Mtumba na mahususi katika shule ya msingi Vikonje” alisema Mwl. Chidumizi.
Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Wanawake katika uongozi, ni chachu kufikia dunia yenye usawa” na katika Jiji la Dodoma yatafanyika katika uwanja wa Nyerere Square.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.