Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kwa jitihada zake za kupambana changamoto ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini, ikiwemo usimamizi wa makao ya Taifa ya watoto Kikombo, Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwenye makao hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo amesema Wizara imefanya jambo kubwa ambalo litasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mhe. Nyongo ameongeza kuwa Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani imekuwa ni changamoto kubwa hivyo ameitaka Wizara kuhakiksha inawasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu na stadi mbalimbali zitakazowasaidia katika maisha yao.
Aidha ameitaka Wizara kuweka mazingira wezeshi hasa kwa watumishi wa Makao hayo kwani wamejitoa katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na makuzi bora.
Pia Mhe. Nyongo amelipongeza Shirika la ABBOTT Tanzania kwa kuona suala la watoto waishio katika mazingira magumu ni muhimu na kuweka fedha kiasi cha shillingi bilioni 2 katika kuhakikisha watoto hao wanakuwa na mazingira mazuri ya kupata malezi na mafunzo mbalimbali.
Mbali na hayo, amempongeza Mhe. Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima kwa jitihada za uelimishaji na uhamasishaji kwa jamii juu ya umuhimu wa kuchanja na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19 ikiwa ni jitihada za Serikali katika kujenga Jamii yenye afya njema ili kukuza uchumi.
Vile vile, Mhe. Nyongo amemtia moyo Dkt. Gwajima na kumtaka kuendelea kuchapa kazi na kumwahidi Bunge kupitia kamati ya kudumu ya Bunge huduma na Maendeleo ya Jamii itaendelea kumpa ushirikiano katika kuboresha Sekta ya Afya nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itasimamia Makao hayo ya watoto ili yaweze kutoa huduma iliyokusudiwa kwa Watoto waliokusudiwa katika Makao hayo.
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Serikali imepokea ushauri uliotolewa na kamati hiyo na kuahidi kutekeleza hoja zote zilizotolewa ili kuboresha huduma kwa watoto wanaoishi katika makao hayo na mengine yote nchini, ikiwemo huduma za kiroho, na michezo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.