KAMATI ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imeishauri Serikali kuweka kipaumbele kwenye kilimo hifadhi kisera na kisheria ili kulinda ardhi na kuwa na kilimo chenye tija.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mahamoud Mgimwa, alisema hayo jana katika kikao cha kamati na wadau wa kilimo kilichohusu mipango na mikakati ya kuendeleza kilimo hifadhi na matumizi ya zana bora za kilimo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Katika kikao hicho, kamati hiyo ilikutana na Shirika la Kilimo Hifadhi Tanzania (CFU) na Mtandao wa Kilimo Hifadhi Barani Afrika (ACTN), ambao wanashauri wakulima kutumia mbinu stahiki za kilimo hifadhi na matumizi sahihi ya pembejeo.
Mgimwa pia alitaka kujua namna serikali ilivyowekeza katika kilimo hifadhi.
"Kilimo hifadhi kina tija na si ndogo kwanza mkulima anapata mazao ya kutosha lakini pia kubana matumizi kwa kuwa matumizi ya mbolea hayatakuwapo kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo kuna tija na hata vyakula vitakavyopatikana vitakuwa vya asili," alisema.
Alieleza hali hiyo itamwezesha mkulima kuuza mazao yake bila kikwazo chochote.
"Kamati itahakikisha serikali wanalipa uzito suala la kilimo hifadhi kwa kuweka sera na sheria, hatuna sababu ya kulikwepa tuliweke watu walijadili," alisema.
Akichangia katika kikao hicho, Mbunge wa Hanang, Mary Nagu, alisema kilimo ndiyo sekta itakayowainua wakulima na awali wakulima wa jimbo lake waliamini kuhusu kilimo hifadhi lakini baadaye walihamasishwa kutumia mbolea za kisasa, hivyo wataalam wana wajibu wa kutoa elimu kwa kina kuhusu hilo.
"Tutawatoaje kwenye matumizi ya mbolea ya kisasa, ili waendelee kuwa na imani, kama mliwaambia mbolea ya kisasa ikitumika kwa muda mrefu inaharibu ardhi kabisa, leo tunawezaje kurudisha hili la kilimo hifadhi kwa wakulima ambapo awali walikuwa wanaamini," alisema.
Nagu alisema suala la kilimo hicho linapaswa kuwa endelevu ili kuwasaidia wakulima na kuwataka wataalamu watoe elimu ya kutosha ili kunusuru ardhi ya Tanzania.
Naye Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, alisema uharibifu mkubwa wa ardhi unafanywa na mbolea na mwamko wa kutumia mbolea ni mkubwa na kuwaomba wataalam kutoa elimu namna ya kurutubisha ardhi kupitia kilimo hicho.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Justine Monko, alisema wataalamu wanashauri mahindi yalimwe na maharage yasiyoliwa ili kuchangia ardhi kupata rutuba lakini elimu zaidi inahitajika kwa wakulima imekuwa ni vigumu kuweka mchanganyiko huo.
Awali, akiwasilisha kwa kamati mada ya uzoefu wa kilimo hifadhi barani Afrika, Mtendaji Mkuu wa ACTN), Mhandisi Saidi Mkomwa, alisema kuna haja ya kubadili kilimo cha sasa kuwa kilimo hifadhi yatakayoendana na matumizi sahihi ya zana za kilimo.
Alisema kuna tatizo kubwa la kilimo cha Tanzania kuchakaza udongo na hivyo kuna haja ya kulinda mazingira kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.
Alibainisha kuwa kuna fursa nyingi zinazojitokeza kwa Tanzania kutokana na mabadiliko yaliyoanza kujitokeza ikiwamo watanzania wengi kuhamia mijini na kwamba ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na watu milioni 35 mijini ambao watategemea kununua chakula.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.