Na.Theresia Francis, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imepongeza mradi wa Soko la wazi la Machinga, ambao ni matokeo ya utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha yanatengwa maeneo maalumu kwaajili ya wafanyabiashara wa biashara ndogondogo maarufu kama Machinga.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Daniel Sillo imetoa pongezi hizo wakati wa zoezi la kukagua mradi huo unaoendelea mkoani Dodoma uliopo eneo la Bahi Road kuanzia mzunguko wa barabara ya kwenda Singida hadi mzunguko wa barabara ya Airport.
“Kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa, ila pia kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na timu yake nzima ya Mkoa wa Dodoma kwa kazi mnayoifanya, sisi kama kamati tunaosimamia mapato ya Nchi tunawapongeza sana” alisema Sillo.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru, alisema soko likikamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara wadogowadogo zaidi ya 2,938 sawa na asilimia 99 ya wafanyabiashara waliohakikiwa ambao ni 3,013.
“Ikifika Tarehe 1 Julai Machinga wote watakua kwenye Soko la Wazi la Machinga, tukikukosa huku tukukute kwenye D Center na sio tena kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwa” alisema Mafuru.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, alisema mradi huu utakua na manufaa kwa jamii, kutakua na jengo la utawala na ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kutoa elimu ya masuala mbalimbali kama vile kodi, ulinzi na usalama, uraia, ujasiriamali na kadharika. Pia kutakua na huduma za awali za matibabu (Huduma ya kwanza).
“Mradi huu umezingatia mahitaji halisia ya kila siku ya machinga, miongoni mwao ni wakina mama, hapa kuna chumba mahsusi cha kina mama wenye watoto wadogo, maalumu kwa ajili ya kuwanyonyesha Watoto na kupumzika, vile vile watu wenye ulemavu miundombinu imewazingatia” alisema Shekimweri.
Aidha kamati hiyo imeshauri ili kuongeza mapato na kupanua wigo wa walipa kodi wafanyabiashara wadogowadogo na wakati warasimishwe ili taasisi mbalimbali za kifedha ziweze kuwakopesha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.