Kamati ya Fedha na Utawala wamekipongeza Kikundi cha Vijana Airsurf kinachojishughulisha na utoaji wa huduma ya TEHAMA ambazo ni huduma ya internet nyumbani na ofisini, usimikaji wa mtandao wa kiambo(LAN), mtandao mpana (WAN) na usimikaji wa kamera za usalama.
Pongezi hizo walizitoa walipofanya ziara katika ofisi za mradi huo kwa lengo la kukagua namna kikundi hicho kinavyoendesha shughuli zake.
Diwani Joan Mazanda Mjumbe Kamati ya Fedha na Utawala alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakijishughulisha na biashara ambazo zimezoeleka masikioni mwa watu, ni nadra kukuta vijana wa rika kama lao wakijishughulisha na biashara ya utoaji huduma ya TEHAMA.
“Nawapongeza sana kwa kutumia taaluma yenu nakuja na mpango wa biashara kama hii. Niwaombe muelekeze nguvu zenu kwenye kujitanganza msiishie kwenye masoko tu, nendeni mbali zaidi nendeni mashuleni na kwenye Taasisi za vyuo wanachuo ndio wanaongoza kwa kutumia intaneti pia mnavyotangaza na kutoa huduma nzuri mnajitengenezea mabalozi wa huduma yenu” alisema Mazanda.
Kwaupande wa Diwani Neema Mwaluko, Mjumbe Kamati ya Fedha na Utawala aliwapongeza kwa uthubutu wa kufungua ofisi na kutumia mkopo waliopewa na halmashauri vizuri hivyo, kuwaomba wajikite katika kutatua changamoto za biashara yao ili waweze kurejesha mkopo waliokopa.
“Nawapongeza sana ninyi ni vijana wa kuigwa. Wapo wanaoomba mkopo lakini wanaishia kugawana hela hawatekelezi lile andiko waliloombea mkopo lakini ninyi mmekuwa waaminifu na imara, msikate tamaa hakuna biashara rahisi. Angalieni namna yakutatua changamoto zenu ili biashara yenu iweze kufanya vizuri muweze kurejesha mkopo wenu kwa wakati, mnaporejesha mnatengeneza mazingira yakuaminika kwa kikubwa zaidi” alisema Mwaluko.
Akisoma taarifa ya mradi, Anna Kasebena Mratibu wa Mradi wa Airsurf, alisema kuwa wanaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mkopo wa asilimia 4 kwa vijana waliweza kupata fedha zilizosaidia katika kutanua wigo wa biashara yao.
Kikundi cha Airsurf kilianza kikiwa na wateja wawili tu, baada ya kupata mkopo tulifanikiwa kufikisha wateja 53 na kuanzisha mradi wa kutoa huduma ya mtandao ijulikanayo kama Airsurf-Hotspot katika eneo la Rehema Nchimbi Complex. Kikundi kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha za kuendeshea mradi kutokana na gharama kubwa zilizopo katika vifaa na uendeshaji wa shughuli za ICT na kutokuwa na ofisi ya kukidhi viwango hivyo, kutoaminika na wateja na wengine kushindwa kabisa kufika ofisini.
Kikundi cha Airsurf ni kikundi cha vijana kilichopo Kata ya Tambukareli jijini Dodoma, kilianzishwa mwaka 2021 na kufanikiwa kupata mkopo wa asilimia 4 wa vijana mwaka 2022 wa kiasi cha shilingi milioni 15.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.