Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeridhishwa na kazi ya usimamizi wa ujenzi wa mabweni na madarasa ya shule ya sekondari Bihawana.
Mwenyekiti wa Kamati Fedha na Utawala iliofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 Daud Mkhandi alisema kuwa usimamizi ni mzuri.
“Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala, nitoe pongezi kwa kazi nzuri ya usimamizi wa ujenzi wa mabweni na madarasa katika shule hii. Lakini pia tulipokuja mara ya mwisho kutembelea shule hii tuliagiza mazingira kuboreshwa ikiwa ni pamoja na kupanda miti na maua. Leo naona mazingira yameboreshwa” alisema Mkhandi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa shule ya sekondari Bihawana, Liberatus Ntilema alisema kuwa shule yake ilipokea fedha za Mradi wa uboreshaji wa elimu ya sekondari (SEQUIP). “Tarehe 24 Mei, 2022 tulipokea fedha shilingi 240,000,000 zilizoelekezwa katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na mabweni mawili yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 80 kila mmoja. Fedha hizo zilitolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI. Shilingi 40,000,000 zilielekezwa kujenga vyumba viwili vya madarasa na shilingi 200,000,000 zilielekezwa katika ujenzi wa mabweni mawili” alisema Ntilema.
Alisema kuwa vyumba viwili vya madarasa vimekamilika na mabweni mawili yamepauliwa. “Kazi zote zilifanywa kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa ujenzi na ushauri wa viongozi waliokuwa wakitembelea kuona maendeleo ya mradi” aliongeza Ntilema.
Mradi huo unalenga kuboresha mazingira ya shule za sekondari kwa kuziongezea uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi ili kuongeza fursa ya wanafunzi wote walioachaguliwa kujiunga kidato cha tano kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya juu ya elimu ya sekondari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.