Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeagiza shule ya msingi Mbabala iliyopo katika Kata ya Mbabala iingizwe kwenye shule zenye mahitaji maalum ili iweze kusaidiwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alipoongoza kamati yake kutembelea na kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo.
Prof. Mwamfupe alisema “hali ya shule siyo nzuri. Shule hii ina msongamano mkubwa wa wanafunzi ni vizuri iingizwe katika shule zenye mahitaji maalum ili iweze kusaidiwa haraka. Tumetaarifiwa kuwa kuna darasa lililoanza kujengwa lakini halikukamilika, ni vizuri darasa hilo likapewa fedha kulikamilisha na walimu waongezwe shuleni hapa ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu”.
Akiongelea mipaka ya shule hiyo, aliagiza shule hiyo ipimwe na kuwekewa alama za mipaka (beacon). Shule hii ikipimwa itaondoa uwezekano wa maeneo yake kuvamiwa na wananchi na kuendeleza shughuli za kibinadamu na kuathiri mwenendo wa kufundisha na kujifunza kwa wanafunzi.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mbabala, Mwalimu Ezra Nathanael alisema kuwa shule yake ilipokea fedha shilingi 40,000,000 zikiwa ni fedha za mapato ya ndani kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa. “Mradi umekamilika hatua zote isipokuwa uwekaji wa vigae kutokana na fedha kuisha. Changamoto katika kutekeleza mradi huu ni kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi. Changamoto nyingine ni uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa, ambapo mahitaji ni vyumba 24, vilivyopo ni saba na upungufu ni 17” alisema Mwalimu Nathanael.
Shule ya Msingi Mbabala ina jumla ya wanafunzi 1,076 baadhi yao wakitembea zaidi ya kilometa tano kwenda shuleni ikiwa na walimu saba na upungufu wa walimu 17 kufikisha mahitaji ya walimu 24.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.