Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepongeza kazi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali.
Pongezi hizo zilitolewa na kiongozi wa timu namba moja ya wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhe. Jaffar Mwanyemba alipokuwa akiongelea ziara iliyofanyika ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.
Mhe. Mwanyemba alisema kuwa kazi zilizofanyika za utekelezaji wa miradi ni nzuri. “Miradi ya ujenzi wa madawati katika shule imetekelezwa vizuri. Tunatakiwa tubadilike, tuwe tunafanya mikutano na wale tunaowapa fedha. Lazima tuwe na maneno makali kidogo kama itatokea kitu ambacho utatofautiana na mwenzako utatiliwa mashaka. Tunaweza kuwashusha vyeo vyao. Hivyo, wengine wataogopa kuwa ukitumia vibaya fedha hizi utakosa cheo jambo litakalowafanya watu kuwa makini kwenye kufanya kazi zao vizuri” alisema Mhe. Mwanyemba.
Kwa upande wake Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fredrick Mwakisambwe alisema kuwa Kamati ya Fedha na Utawala ilitembelea shule mbili za sekondari ya Mlimwa na Dodoma. “Miradi inaendelea vizuri. Kwa upande wa shule ya Mlimwa sekondari, mradi wa vyumba vitatu vya madarasa umekamilika. Kwa upande wa Dodoma sekondari ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vyenye ofisi katikati” alisema Mwalimu Mwakisambwe.
Alisema kuwa fedha ya EP4R shilingi milioni 40 ilitolewa kutekeleza mradi huo. “Tumepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wajumbe na maelekezo yaliyotolewa tunaenda kuyafanyia kazi. Kipekee tumshukuru sana mheshimiwa Rais, pamoja na serikali yake kwa ujumla kwa maana ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, pia Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wakuu wa shule na watendaji ambao kimsingi tunashirikiana kuhakikisha miradi inafanyika na kukamilika kwa wakati na inafanyika kwa ubora wa hali ya juu ili taaluma ya nchi yetu iweze kuwa bora na kuimarika zaidi” alisema Mwalimu Mwakisambwe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.