Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala imeridhishwa na ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Mkonze iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mapato ya ndani.
Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sospeter Mazengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya alisema kuwa kazi ya ujenzi wa madarasa mawili ni nzuri na kuitaja kuwa inaonekana. “Tumekuja kuona na kukagua matumizi ya fedha na utekelezaji wa miundombinu ya madarasa katika shule hii. Lengo la ukaguzi huu ni kuona kwa macho na pale tunaposoma taarifa zenu na kuona zina mashiko tunazifanyia kazi na kutekeleza mapendekezo mnayotoa. Pale tunapozitilia shaka tunaagiza Mkaguzi wa Ndani kufanya ukaguzi katika eneo husika” alisema Mazengo.
Aliagiza ifanyike tathmini ili kupata makadirio halisi ya gharama ya ukamilishaji wa mradi huo. Vilevile, alishauri kuwa ukamilishaji wa mradi huo uwe kwenye vipaumbele vya mpango na bajeti wa kata.
Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa mradi wa nyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Mkonze, Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Andrew Rumishaeli alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 40,000,000.
Mwalimu Rumishaeli akiongelea hatua ya utekelezaji wa mradi alisema kuwa mradi huo umetekezwa kwa asilimia 97. Alisema kuwa kazi zinazotarajia kufanyika ni usukaji wa umeme awamu ya pili na upachikaji wa vioo vya madarasa na shata za milango. “Changamoto katika utekelezaji wa mradi huu ni fedha kutotosheleza kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi kwa asilimia 100 kwa sababu fedha kwa ajili ya vifaa vya umeme kwa awamu ya pili na shata za milango hazijatosha” alisema Mwalimu Rumishaeli.
Aidha, alisema kuwa ujenzi huo unahitaji fedha kidogo ili uweze kukamilika. Alikitaja kiasi cha fedha kinachohitajika kukamilisha ujenzi huo kuwa ni shilingi 2,400,000.
Wakati huohuo, mkuu huyo wa shule alikumbushia kukamilishwa kwa ujenzi wa jengo la utawala lililoanza kujengwa miaka miwili iliyopita. “Kuna jengo la utawala ilishapita miaka miwili ya fedha, tunaomba tusaidiwe kulikamilisha. Tulipewa shilingi 55,000,000 kwa ajili ya ujenzi wake, hadi sasa bado kama shilingi 45,000,000 ili likamilike. Kutokamilika kwa jengo hilo maana yake tunaendelea kutumia madarasa kwa shughuli za kiutawala. Jengo la utawala likikamilika litaachia madarasa yaendelee kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa” alisema Mwalimu Rumishaeli.
Mwenyekiti Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Mohamed Missanga alisema kuwa wakati wa utekelezaji wa ujenzi huo, wanazingatia kuwa vitakuja vizazi vingi kutumia madarasa hayo. “Tunawashukuru kwa kuja kututembelea na kutukagua, dhamira yetu ni ukamilishaji wa mradi, kuusimamia vizuri. Pongezi kwa mkuu wa shule na watendaji kwa kuwa karibu katika utekelezaji wa mradi huu” Missanga.
Shule ya sekondari Mkonze ina jumla ya wanafunzi 1,164, wasichana wakiwa 646 na wavulana 518, ikiwa na walimu 56. Shule hiyo inahudumia mitaa minane ya Kata ya Mkonze ambayo ni Chidachi, Miganga, Chinyika, Bwawani, Chisichiri, Muungano ‘A’, Muungano ‘B’ na Nzinje.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.