WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetakiwa kuhakikisha inatenga bajeti mahususi kwa ajili ya kutoa elimu ya TEHAMA nchini.
Rai hiyo imetolewa na Selemani Kakoso (Mb) ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wa kikao cha kamati kilichohusisha Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari kilichofanyika katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.
Kakoso ameeleza kuwa ulimwengu wa utandawazi umesababisha kusambaa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususani matumizi ya kompyuta na viambata vyake na kuitaka Wizara hiyo kuhakikisha inatenga bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kuwa "Kuwe na mkakati wa maboresho na mpango wa kuhakikisha kuwa elimu ya TEHAMA inaenezwa nchini maana sote lazima tukubaliane kuwa TEHAMA ndio ulimwengu wa sasa."
Kakoso amesema kuwa endapo mapato ya Serikali yatakuwa ni kidogo kuna kila sababu ya kutafuta fedha mahali popote ili kuhakikisha mapinduzi ya TEHAMA yanapatikana nchini.
"Mimi nawahakikishia kuwa bila kujenga vijana wenye teknolojia bora nchi yetu haitakuwa salama, TEHAMA ndio mwarobaini wa maendeleo ya nchi yetu na Dunia nzima imeelekea huko", amesisitiza Kakoso.
Kakoso amepongeza kazi zinazofanywa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kufanya maboresho na usimamizi madhubuti wa miradi ya mawasiliano katika maeneo mengi nchini.
"Nawahakikishia kuwa kama tungetegemea mfumo wa makampuni pekee kusingekuwa na mawasiliano ya kutosha.
Minara mingi imezidiwa hivyo ni vizuri kuendelea kufanya maboresho ili kuondoa changamoto zozote za mawasiliano", ameeleza Kakoso
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.