Na. Dennis Gondwe, MIYUJI
KAMATI ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma imepongeza usimamizi mzuri wa shule mpya inayojengwa ya Miyuji B iliyopo Kata ya Miyuji jijini Dodoma na kusema kuwa shule hiyo itawapunguzia hadha ya kutembea umbali mrefu wanafunzi.
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga alipoongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya Miyuji B inayojengwa Kata ya Miyuji.
Mbaga alisema “nimpongeze mkuu wa shule jirani ya Miyuji anayesimamia ujenzi wa shule hii kwa kazi nzuru na usimamizi mzuri. Hakika majengo ni mazuri na yanapendeza. Aidha, niwapongeze na wahandisi kwa kusimamia vizuri shule hii. Maeneo mengine wahandisi hawasimamii miradi ya ujenzi jambo linalopelekea miradi mingi kujengwa chini ya kiwango kwa kukosa usimamizi”.
Vilevile, kiongozi huyo wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma alielezea kufurahishwa kwake kwa taarifa ya shule kutambua mchango wa nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule hiyo.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa shule mpya Miyuji B, Mkuu wa Shule ya Sekondari Miyuji, Greyson Maige alisema kuwa shule hiyo inakwenda kuwaondolea hadha wanafunzi ya kutembea umbali mrefu na kufika shuleni kwa wakati. Faida za mradi huu utakapokamilika ni kuwasaidia wanafunzi watatembea umbali mfupi na kufika shule kwa wakati. “Faida nyingine ni kupunguza idadi ya wanafunzi Shule ya Sekondari Miyuji ilipo Kata ya Mnadani na kupunguza mimba za utotoni pamoja na utoro wa wanafunzi. Kwa upande wa walimu watakaa kwenye mazingira ya shule na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuwezesha mazingira mazuri ya kuishi kwa walimu” alisema Mwl. Maige.
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo alisema kuwa ulianza kutekelezwa Mwezi Agosti, 2023 baada ya taratibu zote za manunuzi kukamilika na ujenzi unatekelezwa kupitia mfumo wa “Force Account”. “Mradi huu unahusisha miundombinu ifuatayo:- Ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa yenye ofisi mbili, jengo la utawala, maabara tatu na jengo la maktaba. Mingine ni jengo la Tehama, Vyoo vya wanafunzi matundu nane na tanki la maji la ardhini. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 95 ikiwa kazi mbalimbali za umaliziaji zinaendelea ambazo ni upakaji rangi, marumaru na usafi” alisema Mwl. Maige.
Matumizi ya fedha za mradi alisema kuwa Shule ya Sekondari Miyuji ilipokea kiasi cha fedha shilingi 544,225,626 tarehe 30 Juni, 2023 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya katika Kata ya Miyuji iliyopo eneo la Mpamaa kupitia mradi wa SEQUIP (Mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu). “Mpaka sasa kiasi cha shilingi 468,225,626 kimetumika” alisema Mwl. Maige.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa eneo la ujenzi wa shule hiyo limechaguliwa kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwa katikati ya maeneo ya wananchi na karibu na eneo zitakapojengwa nyumba 3,500 na Wakala wa Ujenzi Tanzania.
“Niwapongezi Diwani wa Kata ya Miyuji na Mkuu wa shule ya Miyuji kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hii. Tulishauri pia kisima kuchimbwa katika eneo kwa lengo la kupata maji ya uhakika. Jukumu la wazazi sasa ni kuwapeleka shule watoto wao na kutafsi elimu watakayoipata kwenye fursa ya ajira” alisema Alhaj Shekimweri.
Ikumbukwe kuwa Shule ya Sekondari Miyuji ipo Kata ya Mnadani ambayo inahudumia wanafunzi kutoka Kata ya Mnadani na Kata ya Miyuji. Idadi ya wanafunzi katika shule ya Sekondari Miyuji ni 1,467 kati yao wavulana ni 650 na wasichana ni 817 na ina walimu 65.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.