KAMATI ya kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya ziara katika shule ya Sekondari ya Ntyuka na shule ya Msingi Mtemi Mazengo zilizopo katika Halmashauri hiyo na kukutana na wanafunzi kwa ajili ya kuwapa elimu kuhusu mimba za utotoni na UKIMWI ili waweze kujitunza na kuzingatia masomo yatakayowawezesha kufikia malengo yao katika Maisha.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake Emmanuel Chibago ambaye ni pia ni Naibu Meya wa Jiji la Dodoma walifanya ziara hiyo leo Oktoba 11, 2021 wakianzia shule ya Sekondari ya Ntyuka iliyopo kata ya Ntyuka na baadaye Shule ya Msingi Mtemi Mazengo iliyopo kata ya Ipagala Jijini humo.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati, Naibu Meya Chibago alisema lengo la ziara hiyo kwanza ni kukagua endapo wanafunzi wanafikishiwa elimu juu ya janga la UKIMWI na mimba za utotoni lakini pia kuzungumza na wanafunzi moja kwa moja juu ya changamoto hizo ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa katika kuandaa maisha yao ya baadaye.
“Tumekubaliana kama kamati kuwa, haitoshi kukaa tu ukimbini kila siku kufanya vikao bila kufika kwa jamii ambayo ndiko walengwa ndiyo maana leo tumeamua kufanya ziara ili tutoe elimu na kukagua kama taarifa tunazokutana nazo vikaoni zina uhalisia huku jamii ilipo” alisisitiza Chibago ambaye ni diwani wa Kata ya Matumbulu Jijini Dodoma.
Baada ya ziara katika shule hizo, wajumbe wa kamati hiyo walikutana na kufanya kikao cha ndani kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kuthibiti UKIMWI zilizofanywa katika kipindi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha yaani kuanzia Julai Mosi hadi Septemba 30, 2021.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.