KAMATI ya kudumu ya Kudhibiti UKIMWI ya Halmshauri ya Jiji la Dodoma inafanya ziara ya siku tatu katika Shule mbalimbali za Sekondari Jijini kwa ajili ya kutoa Elimu kuhusu UKIMWI na mimba za utotoni kwa wanafunzi wa kike ili waweze kujilinda na kufikia ndoto zao.
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jumanne Ngede ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamekuwa wakifanya mikutano na Wanafunzi katika Shule hizo na kutoa mada zinazohusu changamoto za Wanafunzi kujihusisha na masuala ya ngono katika umri mdogo.
Akizungumza katika mikutano kwenye Shule tofauti zilizotembelewa na Kamati hiyo, Mwenyekiti Ngede amewataka Wanafunzi hususan wa kike kujiepusha na vitendo vya ngono katika umri mdogo kwani zinaweza kukatisha ndoto zao kwa kupata mimba na kukatisha masomo.
Alisema Kamati anayoiongoza imeamua kuanzisha utaratibu wa kutembelea Shule za Jiji hilo na kutoa Elimu ya UKIMWI na Mimba za utotoni ili kuongeza tija zaidi kwa Wanafunzi ili waweze kufikia malengo yao katika maisha.
Kwa upande wake Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI wa Halmashauri hiyo Daisy Geofrey alisema ziara za Kamati hiyo zitafanyika katika kila kipindi cha robo mwaka kwani hilo ni jukumu la msingi la Kamati hiyo.
Shule za Sekondari zilizotembelewa na Kamati hiyo mpaka sasa ni Mpunguzi, Mbabala, Mkonze, Sechelela, Viwandani, Makole, Chinangali, na Lukindo ambapo mikutano kati ya Kamati hiyo na Wanafunzi imefanyika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.