Kamati za urasimishaji zimeelekezwa kutokuwa miungu watu na badala yake zimetakiwa kusimamia na kuwa kiunganishi kati ya wananchi na wataalamu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) watakaoenda kutekeleza zoezi la urasimishaji katika Jiji la Dodoma.
Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis G. Mwamfupe tarehe 4 Machi 2023 wakati akifungua mafunzo kwa Kamati za Urasimishaji kutoka Mitaa ya Bihawana, Mapinduzi A, Mapinduzi B na Mpunguzi katika ukumbi wa Mkandarasi Jijini Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema ‘‘kamati zilizochaguliwa zinapaswa kutoa ushirikiano mkubwa kwa wataalamu wa mradi ili kutimiza malengo yaliyopo kwa kuwa ni viungo kati ya wataalamu na wananchi na sio kwenda na kujifanya miungu watu na kusahau kuwawakilisha wananchi waliowachagua’’.
Aliendelea kusisitiza kuwa, kamati hizo zina jukumu la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na ni vyema zikashawishi kuondokana na mila potofu hasa kwa wale wanaosema ukipimiwa ardhi inashuka thamani ambapo alisema kuwa hizo ni fikra potofu na zinatakiwa kupingwa kwa sababu unapopimiwa unaongeza thamani na kukupa uhakika wa mipaka yako
‘‘Makazi holela yanawanyima wakazi nchini mwetu kuweza kutumia makazi yao waliyoyajenga kwa shida na kwa kipindi kirefu kama kitu cha kuwasaidia katika mikopo hivyo nchi ikaona kuwa miongoni mwa mambo ya kuwainua wananchi wake ni kutambua makazi yao ili yawe rasmi’’. Alisema Prof Mwamfupe
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.