Na Getruda Shomi, DODOMA
KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda amewaasa wananchi wa Kata ya Dodoma Makulu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi siku ya kufanya sensa ya majaribio ya watu na makazi ambayo inayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 11 hadi 13, 2021 katika Kata hiyo ikiwa ni majaribio ya kupima nyenzo zilizoandaliwa ikiwemo mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) itakayotumika katika zoezi hilo nchi nzima mwakani.
Aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata hiyo uliofanyika katika uwanja wa Ofisi ya Mtendaji wa Kata na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri, Diwani wa Kata hiyo Fadhili Chibago pamoja na Wenyeviti wa Mitaa.
Akiwaeasa wakazi hao kutoa ushirikiano mkubwa kwa mawakala wa sensa ya majaribio na wale watakaofanya sensa rasmi mwaka 2022, Makinda aliwaomba wananchi hao kutoa taarifa sahihi kwa kila swali litakalo ulizwa pasipo kuwa na udanganyifu wowote ili Serikali ipate taarifa sahihi kuhusu watu na makazi, lakini pia sensa ni siri na mawakala hao wameapa kutunza siri.
“Zoezi la sensa ni la siri na litafanyika kwa siri, tunaomba muondoe hofu” alisema Makinda.
Akizungumzia lengo la zoezi la sensa ya watu na makazi, Kamisaa Makinda alisema ni kutambua idadi ya watu nchini, kujua ubora wa nyumba, kiwango cha umaskini na maendeleo, lakini pia nyumba kupewa anuani kwa lengo la kutambua wakazi wa kaya husika.
Alisema idadi ya mikoa iliyotengwa kwa ajili ya sensa ya watu na makazi ya majaribio ni 18, ikiwemo mitano ya Zanzibar na kwa Tanzania Bara ni Mikoa 13.
Awali wakati akimkaribisha Kamisaa Makinda, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri alisisitiza kuwa, sensa ya watu na makazi ni muhimu na kila mwananchi ni haki yake kuhesabiwa ili kutambulika na serikali.
Sensa ya watu na makazi itafanyika rasmi mwaka 2022 ikiwa ni sensa ya sita tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961 na hufanyika kila baada ya miaka kumi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.