HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefanikiwa kuchanja watoto 34,981 katika siku mbili za utekelezaji wa kampeni ya kitaifa la chanjo ya Surua Rubella na Polio.
Takwimu hizo zimetolewa na mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji Dkt. Gatete Mahava alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya Surua Rubella na Polio kwa siku mbili za utekelezaji wa kampeni hiyo ya siku tano.
Dkt. Mahava alisema kuwa jumla ya watoto 34,981 walichanjwa kwa siku mbili za mwanzo za utekelezaji wa kampeni hiyo. “Watoto waliochanjwa kujikinga na Surua ni 22,768 sawa na asilimia 41. Aidha, watoto waliochanjwa dhidi ya kujikinga na Polio ni 12,213 sawa na asilimia 35” alisema Dkt. Mahava.
Mganga mkuu huyo aliwahakikishia wananchi kuwa chanjo hizo ni salama na kuwataka kupuuza taarifa zozote zinazolenga kupotosha ufanisi wa kampeni hiyo.
Wakati huohuo, Hawa Ramadhani mzazi aliyepeleka mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu na miezi tisa kupatiwa chanjo alielezea furaha yake baada ya mtoto wake kupatiwa chanjo hiyo. “Ninafuraha leo mtoto wangu amechanjwa ili kumkinga na ugonjwa wa Surua katika hiki kituo cha Afya Makole. Wito wangu wazazi na walezi wajitokeze kuwapeleka watoto wakapatiwe chanjo za aina zote kulingana na umri wao” alisema Ramadhani. “Chanjo ni muhimu sana kwa kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa ya Surua na Polio, unaona hata mganga mkuu wa Jiji letu leo siku ya mapumziko lakini anapita kwenye vituo kukagua jinsi zoezi hili linavyoendelea” alisema mama huyo.
Kampeni ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua Rubella na Polio katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza tarehe 17/10/2019 na itaendelea hadi tarehe 21/10/2019, ikiongozwa na kaulimbiu isemayo “Chanjo ni Kinga, kwa Pamoja Tuwakinge”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.