Na. Josephina Kayugwa, DODOMA.
MWENYEKITI wa Mabalozi wa Sauti ya Wapinga Rushwa Mkoa wa Dodoma, Haruna Kitenge, amezindua kampeni ya “Sepesha Rushwa marathon” yenye lengo kujenga uelewa wa jinsi gani ya kupinga rushwa na kuhamasisha sauti za jamii nchini Tanzania.
Kampeni hiyo imezinduliwa katika uwanja wa mpira wa miguu Jamhuri Dodoma ambapo Mwenyekiti huyo amesema vijana ndio Taifa la kesho hivyo wanatakiwa kuelimishwa juu ya madhara ya rushwa kwa sababu rushwa ni adui wa haki.
“Kwa mwaka 2022 mbio hizi zitafanyika Jumapili tarehe 11 Disemba, katika jiji la Dodoma. Mbio hizo zinatarajia kujumuisha washiriki zaidi ya 2,000 kutoka Tanzania nzima, hivyo vijana wahamasike kushiriki ili tuweze kuelimishana kuhusu madhara ya rushwa.
Usajili umeanza rasmi tarehe 16/9/2022 na unafanyika kupitia tovuti yetu ya www.anticorruptionvoices.or.tz au www.eventbrain.com ambapo katika tovuti hizi utakuta ukurasa wa Sepesha Rushwa Marathon na usajili utafanyika kwa awamu tatu kwa gharama tofauti kulingana na awamu yako utakayoamua kujisajili,” alisema Kitenge.
Aidha, alisema kuwa anawaomba wadau na taasisi mbalimbali kuunga mkono ili kuweza kufikisha ujumbe sehemu mbalimbali na kuisaidia Serikali juu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Lakini pia alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweli na Serikali nzima ya Jiji la Dodoma kwa kuwaunga mkono katika uzinduzi wa kampeni ya “Sepesha Rushwa Marathoni”.
Kwa upande wake Katibu wa riadha Mkoa wa Dodoma Robert Mabonye, amesema Wilaya zote zijitokeze kushiriki mbio hizi ili kusambaza ujumbe Tanzania nzima.
“…nawashauri watu wote katika kushiriki mbio hizi kwa sababu mazoezi ni afya lakini pia ni kwa lengo la kupambana na Rushwa na kuitokomeza zaidi,” alisema Mabonye.
Katibu wa riadha Mkoa wa Dodoma Robert Mabonye (aliyesimama) alipokuwa akiongea wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya 'Sepesha Rushwa Marathoni' jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.