Na. Josephina Kayugwa, DODOMA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amezindua kampeni ya usalimishaji wa silaha haramu yenye lengo la kukusanya silaha zote ambazo zinamilikiwa kinyume na sheria za nchi.
Kampeni hiyo imezinduliwa leo katika uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma ikiongozwa na kauli mbiu inayosema “Silaha haramu sasa basi salimisha kwa hiari”.
Akizungumza katika uzinduzi huo alisema kila mwananchi anawajibu wa kutoa taarifa katika chombo chochote cha Jeshi la Polisi, ikiwa mtu yoyote ataonekana anamiliki silaha kinyume na taratibu za nchi.
“Wananchi wanatakiwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa amani, kama silaha haramu zikizagaa ndipo uharifu unaongezeka nchini. Kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi zote tunaamini kampeni hii itafanikiwa. Pia katika kipindi hiki cha msamaha hakuna adhabu yoyote ambayo itatolewa kwa mtu atakayesalimisha silaha anayoimiliki kinyume na sheria” alisema Sagini.
Aidha, aliomba ushirikiano kwa Polisi Jamii, viongozi wa mitaa, vyombo vya habari pamoja na mashirika ya kijamii yote kutoa elimu kipindi hiki ambacho msamaha umetangazwa ili zoezi lifanikiwe.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Camilius Wambura alisema Jeshi limejipanga vizuri, kampeni itaendeshwa nchi nzima ikihusisha kufanya mikutano na kutoa elimu, viongozi wa mitaa na Jeshi la Polisi watashirikishwa katika zoezi la kukusanya silaha.
“Kampeni ilianza tarehe 1 Septemba, 2022 na itahitimishwa 31 Oktoba 2022. Tunaimani katika muda wa msamaha kila anayemiliki silaha ataisalimisha katika uongozi wa sehemu anayoishi kisha silaha hiyo kusalimishwa kituo cha polisi, tukio la kuteketeza litafanyika kwa uwazi mwezi Novemba ili wananchi washuhudie jitihada za Serikali katika kuhakikisha Tanzania inabaki salama,” alisema IGP Wambura.
Aliongezea kwa kusema “Nawakumbusha wamiliki wa silaha wazingatie sheria na kanuni ili silaha zisiangukie mikononi mwa wahalifu na kubadilika kuwa haramu kitu kitakachosababisha kufutiwa leseni ya umiliki.
Alimalizia kwa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa msamaha ili silaha haramu zisalimishwe zoezi litakalosaidia kuimarisha amani na utulivu wa nchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.