WAZIRI wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amezindua kampuni mpya ya PASS Leasing Company LTD inayomilikiwa na Taasisi ya PASS Trust yenye lengo la kutoa mikopo ya zana za kilimo bila dhamana yoyote kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Akizungumza leo Julai 24,2021 kwenye viwanja vya 'Nyerere Squre' jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampuni hiyo pamoja na ufungaji wa wiki ya Taasisi ya PASS Trust (Private, Agriculture Sector Support Trust) iliyoandaliwa na Taasisi hiyo kuanzia Julai 21 hadi Julai 24 kwa lengo la kuchagiza masuala ya kilimo nchini.
Prof. Mkenda amesema kuwa lengo ya wiki ya PASS lilikuwa ni kuwakutanisha wadau wa kilimo wakiwemo wakulima wenyewe, wauzaji wa zana za kilimo, taasisi za kifedha, wauzaji pembejeo, viongozi wa Serikali na wachakataji ili kuzungumzia maswala ya upatikanaji wa fedha kama kichocheo cha ukuaji wa kilimo biashara.
“PASS imekuwa itoa dhamana ya mikopo kuanzia asilimia 20 -60 na hadi asilimia 80 kwa wanawake kwa benki shiriki kama njia ya kuongeza dhamana ya kutosha ili kuwezesha wateja kupata mikopo,” amesema.
Vile vile, ameipongeza PASS kwa kuandaa wiki hiyo na kuwakutanisha wadau mbalimbali na kuwataka kwenda kujifunza zaidi na kuwa bora kutokana na kongamano hilo.
Aidha amesema kuwa Serikali inatarajia kuleta mbegu bora za alizeti na kuzigawa kwa mkataba kwenye viwanda vinavyozalisha zao hilo hali itakayofanya soko hilo kuwa la uhakika na kuondoa uhaba wa Mafuta unaojirudia kila Mwaka.
“Serikali itawajibika kwa kuwawezesha wakulima kwa kuwapelekea wataalamu wa zao la alizeti, na tutaweka masharti kuwa ukivuna alizeti unamuuzia mwenye kiwanda ili kuhakikisha viwanda vyote vinavyoingia mkataba vinazalisha mafuta kwa mwaka mzima,” amesisitiza Waziri Mkenda.
Prof. Mkenda ametumia nafasi hiyo kuzitaka Benki zote nchini kutoa fursa ya mikopo kwa wakulima na kushusha riba ili kuchochea kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima wengi zaidi kukifanya Kilimo kuwa biashara.
“Ukitaka kupambana na umaskini Tanzania, unaweza kufanya mambo mengi sana lakini ukweli ni kwamba umaskini utaisha kwa kilimo, ukitaka mali utaipata shambani,” alikumbusha Waziri akinukuu maneno kutoka kwenye moja ya mashairi ya zamani.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo Dkt. Tausi Kida amesema kuwa changamoto za mitaji kwa wakulima nchini bado zipo nyingi na kwamba ipo haja kwa Taasisi za fedha kuongeza kiwango kwa wakulima. “Ili kuweka tija kwenye mazao ya kimkakati tunapaswa kuongeza nguvu katika kukuza zao la alizeti na zabibu ili kusaidia viwanda vya uchakataji, kwa upande wetu tumeanza na programu kwa mikoa ya Simiyu, Dodoma, Singida na Morogoro kwa kutoa pembejeo,” amefafanua Dkt. Kida.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema ili kufanikisha maendeleo ya Kilimo Mkoani hapa wanatarajia kusajili Kaya laki 3 zinazostahili kufanya kilimo biashara na kuwa fahari kwa jiji hili. ”Mazao ya zabibu na alizeti kuwa ya kimkakati, na ili kufanikisha hilo nitatumia nafasi yangu kwa kushauriana na Wizara ya kilimo kuona namna ya kuongeza ufanisi kwa mazao hayo” amesema Mtaka.
Waziri wa Kilimo.Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampuni Mpya ya PASS Leasing, hafla iliyofanyika kwenye kufunga Wiki ya PASS Trust kwenye viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya PASS Trust, Dkt. Tausi Kida akizungumza wakati wa Uzinduzi huo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Athony Mtaka,akizungumza wakati wa uzinduzi wa PASS Leasing ambapo alielezea mikakati ya Mkoa wa Dodoma katika kutumia fursa ya utekelezaji wa uzalishaji mazao ya kimkakati ya Zabibu na Alizeti.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.