Na. Dennis Gondwe, DODOMA MAKULU
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya msingi inayoendelea katika Shule ya Msingi Kisasa kupitia Mradi wa Kuboresha Upatikanaji wa Fursa sawa katika Ujifunzaji bora wa Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST).
Kauli hiyo aliitoa alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Kisasa iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Tumetembelea Shule ya Msingi Kisasa na tumeshuhudia madarasa mawili yakiwa kwenye hatua nzuri sana ya upauaji na vyoo vinaendelea kujengwa. Kwa kweli tumefurahishwa sana na kasi ambayo tumeiona. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mkurugenzi wa Jiji na wote wanaohusika kusimamia mradi huo akiwemo mwalimu mkuu na kamati yake inayofanya kazi hiyo. Kazi ni nzuri na tumehimiza umaliziaji uendane na muda uliobaki” alisema Senyamule kwa tabasamu la uhakika.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisasa, Jesca Mwarabu alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 63,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano, matundu sita ya vyoo na kutengeneza samani. “Mradi huu unatekelezwa na kusimamiwa na kamati tatu zilizoundwa ambazo ni kamati ya ujenzi, kamati ya manunuzi na kamati ya mapokezi na ukaguzi wa vifaa. Mpaka sasa ujenzi umefikia hatua ya kupiga plasta kwa madarasa yote mawili na kufunga renta katika jengo la choo. Mpaka sasa malipo yaliyofanyika ni shilingi 40,131,250 tunatarajia ifikapo tarehe 10 Juni, 2023 kazi hii iwe imekamilika kwa asilimia 100” alisema Mwarabu.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akiambatana na kamati yake ya Usalama alifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya elimu katika Jiji la Dodoma akianzia Shule ya Sekondari Bunge, Shule ya Msingi Kisasa, Shule ya Msingi mpya inayojengwa Swaswa na Shule ya Msingi mpya inayojengwa Mbwanga, Mkuu wa Mkoa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.
Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano unavyoendelea katika Shule ya Msingi Kisasa iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.