Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO
KATA ya Chamwino imetakiwa kusimamia utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa mujibu wa maelekezo ya serikali ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe Mtaa wa Mailimbili aliyofanyika katika mtaa wa Mailimbili.
Ngede alisema kuwa ni jambo zuri kwa wataalam na Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamwino kusimamia suala la Lishe kutokana na umuhimu wake katika jamii. Alisema kuwa kutokana na umuhimu wake, serikali ilisaini mkataba wa Lishe na makundi mbalimbali ili watekeleze mkataba huo kwa kuhakikisha elimu ya Lishe inatolewa na utekelezaji wa mkataba huo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alisema kuwa suala la utekelezaji wa mkataba wa Lishe ni maelekezo ya serikali yanayotakiwa kutekelezwa kwa uzito mkubwa. “Tumeshasaini mkataba wa Lishe, utakumbuka Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisaini mkataba na wakuu wa mikoa. Wakuu wa mikoa wakasaini na wakuu wa wilaya. Wakuu wa wilaya wakasaini na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, nao wakasaini wa maafisa watendaji wa kata. Maafisa watendaji wa kata wakasaini na maafisa watendaji wa mitaa. Hii inaonesha umuhimu wa masuala ya Lishe na afua zake katika jamii. Lengo kubwa ni kupunguza athari za utapiamlo katika jamii” alisema Nkelege.
Alisema kuwa huduma zilizotolewa katika maadhimisho hayo ni elimu ya Afya na Lishe, maonesho ya makundi matano ya vyakula na upikaji wake, upimaji wa Afya ukihusisha kupima HIV, uzito na urefu (BMI) pamoja na kutoa kutoa vyeti kwa watoto wadogo, matone ya Vitamin "A" na kupima MUAC kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Afisa mtendaji huo alisema matarajio ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe, alisema kuwa ni kuona hali ya lishe inabadilika na kuwa bora zaidi katika kata yake hasa kwa kina mama wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na vijana balehe.
Akiongelea maadhimisho hayo alisema kuwa ni utekelezaji wa kipengele namba mbili katika mkataba wa lishe linachoelekeza kata na mitaa kufanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIKI) katika mitaa.
Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ya Mtaa hufanyika kwa mitaa yote kila baada ya miezi mitatu na katika mtaa wa Mailimbili yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Lishe Bora kwa Ustawi wa Afya zetu na Maendeleo ya Mtaa wetu” ukiwa ni mtaa wa pili ukitanguliwa na mtaa wa Sokoine.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.