Na. Shaban Ally, DODOMA
KATA ya Chang'ombe imempongeza Diwani wake Mhe. Bakari Fundikira kwa juhudi zake za kuleta maendeleo katika kata hiyo kwa kutatua changamoto za afya na elimu.
Pongezi hizo zimetolewa na Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Emmanuel Mazumila (aliyesimama pichani juu) wakati akimkaribisha diwani kufunga kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kilichofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata leo tarehe 02 Juni, 2022.
Mazumila amesema kuwa anampongeza diwani wa kata hiyo kwa kutatua changamoto ya afya na elimu. Amesema kuwa diwani huyo amekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe na kuwaondolea kero ya kutembea umbali mrefu wananchi kufuata huduma za afya. Katika elimu alisema kuwa diwani huyo ameshiriki kuhimiza wazazi kuwapeleka watoto shule na kufuatilia maendeleo yao, aliongeza Mtendaji huyo.
Aidha, Mazumila amewashauri wananchi na wadau wa maendeleo katika Kata hiyo kuendelea kuheshimu na kuthamini juhudi zinazoendelea kufanywa na diwani wao katika kuwaletea maendeleo. Mtendaji huyo ameshauri jina la diwani huyo liwekwe kwenye moja ya barabara au mtaa katika kata yao kama wafanyiwavyo viongozi mbalimbali.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Mhe. Bakari Fundikira aliwashukuru viongozi na wananchi wa Kata ya Chang'ombe kwa pongezi walizompatia juu ya kazi kubwa anayoifanya ya kutatua changamoto zilizopo katika kata hiyo kwa muda mrefu. "Mimi binafsi nimepokea pongezi hizi kwa moyo mkunjufu kwa kuwa bila ya mshikamano wetu, sisi kama viongozi, hatuwezi kufanikisha masuala ya kimaendeleo," alisema Fundikira.
Kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Chang’ombe kilihudhuriwa na Wenyeviti wa Mitaa, Mabalozi, wadau wa maendeleo na wajumbe. Pamoja na mambo mengine kikao kilijadili masuala ya afya na elimu katika kata hiyo.
Mheshimiwa Bakari Fundikira (katikati) akishukuru kwa pongezi alizopewa kutokana na juhudi zake za kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za afya na masuala ya elimu katika kata ya Chang'ombe.
Baadhi ya Wenyeviti wa Mitaa, Mabalozi, wadau wa maendeleo na wajumbe wa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kilichofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata leo tarehe 02 Juni, 2022.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.