Na. Abdul Juma, DODOMA MAKULU
Mkopo wa mapato ya ndani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma usio na riba wa shilingi 328,800,000 umewawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi katika kata ya Dodoma Makulu.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Dodoma Makulu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sophia Abdallah alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mikopo ya mapato ya ndani iliyokopeshwa kwa wanavikundi wa kata hiyo kwa kipindi cha serikali ya awamu ya sita.
Alisema kuwa serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka minne imewezesha vikundi vya wanawake 21, vikundi vya vijana vitatu na vikundi vya watu wenye ulemavu sita kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao. Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa fursa kwa vijana kufanya biashara mbalimbali katika kata hiyo. “Baadhi ya vikundi vimeweza kununua bajaji na pikipiki ili kufanya biashara ya usafirishaji wa abiria kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma kwenda Sabasaba. Eneo la marejesho, vikundi vimefanya vizuri kurejesha kwasababu wamelipa kabla ya wakati kufika. Vikundi vingine vimeweza kuomba tena mkopo kwa awamu hii inayotarajiwa kukopeshwa tena. Hivyo, nivipongeze vikundi hivi na waendelee kuwa na juhudi zaidi” alipongeza Abdallah.
Kwa upande wake, mnufaika wa mkopo wa asilimia 10, Nazalena Kufakunoga alieleza namna mkopo ulivyoweza kumnufaisha katika shughuli zake za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kueleza alivyopata faida na kufungua duka linalouza bidhaa za matumizi ya nyumbani.
“Mkopo huu, tulichukua kwa kikundi tukanunua ng’ombe, faida iliyopatikana tukafungua duka na sasa tunatarajia kuongeza ng’ombe wengine. Naipongeza serikali kwa kuendelea kutuwezesha akina mama na makundi mengine kwasababu zamani tulikuwa chini ila kwa sasa tumeinuka kiuchumi. Tumeweza kujikwamua kwasababu tunasomesha watoto kupitia matokeo ya mkopo huu wa asilimia 10” alieleza Kufakunoga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.