Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na uboreshaji mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Kata ya Hombolo Makulu baada ya kupokea shilingi milioni 470 kupitia mradi wa SEQUIP.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Sekondari wa Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa SEQUIP unaotekelezwa kwenye eneo la Elimu ya Sekondari kuanzia kidato cha 1 – 6 kwa muda wa miaka mitano (5) kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025 nchi nzima na utekelezaji wake umeelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali yanayogusa moja kwa moja elimu ya sekondari. Shule mpya za sekondari 1,000 zinajengwa nchini katika kata ambazo hazina shule za sekondari na maeneo ambayo yana wanafunzi wengi ukilinganisha na miundombinu iliyopo.
Amesema kuwa mradi huo unahusisha pia ujenzi wa shule mpya za sekondari za wasichana za mikoa 26 ambapo kila mkoa inajengwa shule moja.
“Hadi sasa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepokea awamu ya kwanza kiasi cha shilingi 470,000,000 (milioni mia nne na sabini) za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma Makulu. Ujenzi huu unahusisha vyumba nane vya madarasa, maabara tatu za sayansi (kemia, biolojia na fizikia), jengo la utawala, maktaba, chumba cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Matundu 20 ya vyoo vya wanafunzi (wasichana matundu 10 na wavulana matundu 10), tanki la maji la lita 10,000, ujenzi wa nguzo ya kuwekea tanki, Ujenzi wa miundombinu ya kunawa mikono na miundombinu ya kuvuna au kuunganisha maji”, alisema Mwalimu Rweyemamu.
Mradi huo umelenga kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu ya sekondari, kuweka mazingira salama ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanapata elimu bora ya sekondari. Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wasiopungua 400 kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Nne, aliongeza Mwalimu Rweyemamu.
Naye Issa Kambi, Afisa Elimu maalum katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, akiwa katika eneo la mradi alisema “ujenzi katika mradi huu ulianza rasmi mwezi Januari mwaka huu, na kama unavyoona ujenzi upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji wa majengo yote”.
Kiasi cha shilingi 408,000,000 (milioni mia nne na nane) kimeshatumika na awamu hii ya kwanza ya ujenzi inatarajiwa kukamilika tarehe 30 Mei, 2022 na awamu ya pili ya mradi huu itahusisha ujenzi wa nyumba za walimu na ununuzi wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Mafundi wakiendelea na ukamilishaji wa jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Moja ya majengo ya maabara ya sayansi likiwa katika hatua ya ukamilishaji.
Madarasa yakiwa katika hatua ya umaliziaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.