Na. Nancy Kivuyo, IPALA
Hamasa ya serikali katika michezo nchini ni kichocheo cha wananchi wa Kata ya Ipala kupenda kushiriki michezo ya aina mbalimbali kwa ajili ya kujenga na kuboresha afya zao ili waweze kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya michezo katika Kata ya Ipala walipotembelea kata hiyo.
Diwani Magawa alisema kuwa serikali imekuwa inafanya hamasa kubwa katika michezo hali iliyopelekea kata yao kuwa na mwamko mkubwa katika kushiriki mashindano mbalimbali yanayoandaliwa katani hapo. “Kwakweli, mambo ya michezo tunaenda nayo vizuri, kila mwaka tunafanya mashindano yanayoitwa ‘Magawa Cup’ ambayo diwani ndiye mimi na kwa kushirikiana na mheshimiwa mbunge tuna ‘Mavunde Cup’, tunaandaa mashindano hayo ili kuwasogeza wananchi karibu zaidi na michezo. Wakati mwingine tunaunganisha michezo na kampeni za kijamii za serikali ili kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja. Yote hii ni katika kuiwezesha jamii kujitambua na kuishi katika ile misingi ya utanzania. Kikubwa zaidi michezo inasaidia kujenga na kuimarisha miili ya wanamichezo” alisema Magawa.
Akaongeza kuwa wataendelea kuandaa mashindano na kuibua vipaji vya michezo ili kuchochea wigo wa jamii kupenda michezo. “Michezo ni afya, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuhamasisha kuboresha michezo katika maeneo yetu. Ukiangalia fedha na zawadi anazotoa kwa timu zetu hapa nchini na makundi mengine, inatia hamasa sana kwamba tukikazania jamii yetu huku chini kupenda michezo itawasaidia huko mbeleni kufanya vizuri ndani na nje ya nchi. Tunaamini wakati mwingine tutaboresha vipengele ili kuwavuta watu wengi kujumuika pamoja na kuijenga Ipala imara kimichezo” alimalizia Magawa.
Nae Mtendaji wa Kata ya Ipala, Herman Malindila alisema kuwa michezo inaunganisha jamii na kupitia michezo wamekua wakitoa elimu mbalimbali kulingana na wakati kwa lengo la kuijenga jamii iliyo bora katika kata hiyo. “Hapa katani michezo imekua ikileta hamasa kubwa. Tumeendelea kuimaisha mahusiano mazuri miongoni mwetu na hili tutaliendeleza chini ya mbunge wetu na diwani” alimaliza Malindila.
Kwa upande mwingine, mkazi wa Kata ya Ipala, Amos Mdabuko, alimshukuru Mbunge Anthony Mavunde na Diwani George Magawa kwa kuendeleza michezo katika kata yao na kusema “nawashukuru sana viongozi wetu, wamekua mstari wa mbele kuhamasisha jamii kushiriki na kupenda michezo. Jamii sasa hivi imeanza kuwa na mwamko wa kupenda michezo, ndugu mwandishi, haya mashindano yakianza watu wanajaa sana kushiriki, ninaamini mashindano ya awamu hii yatakua makubwa na ya kuvutia”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.