Na. Nancy Kivuyo, MAKUTUPORA
Kata ya Makutupora yapongeza juhudi za serikali ya awamu ya sita za kuboresha miundombinu ya michezo jambo iliyopelekea hamasa kwa wananchi kupenda kushiriki katika michezo kwaajili ya kuibua vipaji na kuboresha afya zao.
Pongezi hizo zilitolewa na Afisa Mtendaji Kata ya Matukupora Hamis Jigwa mbele ya waandishi wa habari waliofanya mazungumzo nae baada ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Alisema kuwa kwenye sekta ya michezo Kata ya Makutupora ina vikundi vya ngoma za asili ambavyo vimekuwa vikishiriki kwenye upokeaji wa Mwenge wa Uhuru na kushiriki mikutano ya kitaifa pamoja na timu za mpira wa miguu. “Hapa katani kwetu tupo vizuri, wananchi wa kata hii wanapenda michezo sana. Hata hii leo kuna mashindano yanaendelea, kama mtapata muda mtaona jinsi wananchi wa hapa wanavyojitokeza kwa wingi kushiriki katika michezo” alisema Jigwa.
Akiongelea chachu ya hamasa ya michezo, alimtaja Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni kielelezo na chachu ya hamasa ya michezo. “Kama mnavyoona ndugu waandishi kuna mashindano yanaendelea hapa, kupitia kampuni iitwayo JBM Ramadhani Cup ambayo yana zawadi nzuri na yana lengo la kuunganisha wananchi na kujenga afya ya mwili” aliongeza Jigwa.
Alimalizia kwa kusema kuwa Kata ya Makutupora ipo mbioni kuandaa mashindano kwaajili ya kuhakikisha vijana wanaonesha vipaji vyao. “Mashindano hayo tutaweka vituo viwili na bingwa wa kila kituo atapata zawadi ya mbuzi na baadae vile vituo viwili bingwa wa kituo ‘A’ na bingwa wa kituo ‘B’ watacheza mechi mbili nyumbani na ugenini na bingwa atapata mbuzi. Kwahiyo, sisi kwetu suala la michezo tumelipa kipaumbele sana” alisisitiza Jigwa.
Nae, mwananchi wa Kata ya Makutupora, Julias Twaja aliipongeza serikali kwa msukumo wa kuboresha eneo la michezo kwasababu linawafanya watoto na vijana kuchangamkia fursa ya kuvumbua vipji vyao. “Michezo katika miaka ya karibuni imekuwa ni ajira nzuri sana kwa watoto na vijana wetu. Ofisi ya kata inafanya vizuri katika kuhamasisha michezo, tuna timu nyingi sana ukanda huu, tunaamini kwa siku zijazo Makutupora tutang’ara katika sekta ya michezo kiujumla” alipongeza Twaja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.