Na. Dennis Gondwe,
KATA ya Mkonze imeanza kutoa mafunzo kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa bila riba na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwajengea uelewa wa uwepo wa mikopo hiyo na taratibu za kuipata.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mkonze, Theresia Camilius wakati akitoa mafunzo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Mkonze iliyopo Kata ya Mkonze Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Theresia alisema kuwa mafunzo hayo yanahusisha vikundi vilivyosajiliwa na vinavyotarajia kuomba mkopo, vikundi ambavyo havijasajiliwa na vinatarajia kuomba mkopo ili viweze kufahamu mchakato na kufanya usajili na kuomba mikopo ya asilimia 10. “Matarajio ya mafunzo haya ni walengwa na wanufaika wa mikopo hii waweze kuelewa fedha zinazotengwa kila robo ya mwaka na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambazo ni asilimia 10 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili. Kwa kuwa mikopo hii ilisimamishwa kwa muda ili kufanya maboresho ya miongozo na kanuni yaliyolenga kuwanufaisha watu wengi zaidi” alisema Theresia.
Alisema kuwa mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yanalenga kuwawezesha kuandika maandiko ya miradi na uandaaji wa katiba za vikundi. Mafunzo yataendelea kwa kipindi cha wiki sita mfululizo yakihusisha pia namna nzuri ya uendeshaji wa miradi na biashara, aliongeza.
Mafunzo hayo yalihusisha jumla ya vikundi 23, kati yake, vikundi 13 vya wanawake, vikundi nane vya vijana na vikundi viwili vya watu wenye ulemavu yakiwa ni mafunzo endelevu hata baada ya vikundi hivyo kuhitimu mafunzo hayo yaliyogawanyika katika sehemu mbili ambazo ni mafunzo kabla ya kuomba mkopo na mafunzo baada ya kuomba mkopo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.