MKURUGENZI wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa, asilimia 63.7% ya kaya zote nchini Tanzania zimefanikiwa kuwa na vyoo bora kwa mwaka 2020, kutoka asilimia 59 mwaka 2019, huku lengo likiwa ifikapo mwaka 2030 kila mtu Duniani atumie choo bora.
Dkt. Subi amesema hayo juzi (Novemba 21, 2020) wakati akiongea na Waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma ikiwa ni siku ya matumizi ya choo Duniani na wiki ya usafi wa mazingira Tanzania.
"Kaya zenye vyoo bora zimeongezeka kutoka asilimia 59 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 63.7 mwezi Juni, 2020, huku lengo namba 6.2 la dunia la maendeleo endelevu limeweka bayana kila mtu Duniani anatakiwa kutumia choo bora huku likitanabaisha kuwa kufikia mwaka 2030 hakuna atakayejisaidia hovyo katika mazingira yasiyo rasmi". Amesema Dkt. Subi.
Amesema kuwa, Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Zingatia Mahitaji ya Jinsia kwa Usafi wa Mazingira Endelevu” (Gender Consideration a Pillar for sustainable Sanitation and Hygiene), lengo likiwa ni kuongeza uelewa zaidi juu ya umuhimu wa kujenga na kutumia choo bora pamoja na kuweka mazingira safi wakati wote.
Aidha Dkt. Subi amesema kuwa, Mikoa inayoongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya kaya zenye vyoo bora ni pamoja na Dar es Salaam (95.8%), Iringa (77.5%) na Njombe (74.6%), huku akiweka wazi Mikoa yenye hali duni ni pamoja na Kigoma (49.3%), Lindi (49.2%) na Dodoma (46.1%).
"Mikoa inayoongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya kaya zenye vyoo bora ni Dar es Salaam (95.8%), Iringa (77.5%) na Njombe (74.6%). Mikoa yenye hali duni ni Kigoma (49.3%), Lindi (49.2%) na Dodoma (46.1%)" amesema Dkt. Subi.
Mbali na hayo, Dkt. Subi amehimiza Jamii ihakikishe inajenga na kutumia vyoo bora ili kuepuka kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko na kuwataka kujenga tabia ya kunawa mikono pamoja na kuimarisha usafi wa mazingira ngazi ya kaya.
Hata hivyo, Dkt, Subi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatupa kinyesi cha watoto chooni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Tovuti hii ilimtafuta Afisa Afya wa Jiji la Dodoma Abdallah Mahia ili kupata maelezo zaidi kuhusu hali ya vyoo katika Jiji la Dodoma ambapo alisema "Hali ya Vyoo bora katika Jiji la Dodoma hatuko kwenye nafasi mbaya, tuna asilimia 76.5 ya kaya zenye Vyoo bora. Kikubwa kilichofanya mkoa wa Dodoma kuwa na kiwango duni imechangiwa na baadhi ya Halmashauri ambazo kiwango chake cha kaya zenye Vyoo bora bado kiko chini sana hivyo kusababisha mkoa kushika nafasi ambayo si nzuri" alifafanua Mahia.
Aidha, Afisa Afya huyo wa Jiji aliwakumbusha wananchi wa mkoa wa Dodoma kujenga Vyoo kwa kutumia vifaa vya kudumu na kuezeka kwa kutumia kenchi (mbao na fito) badala ya kuweka bati au nyasi pekee na kupelekea mvua zinaponyesha Vyoo hivyo kuanguka na kubaki wazi sehemu ya juu na hivyo kupoteza ubora wa vyoo hivyo. Bwana Mahia amesisitiza kuwa jambo hili ni jukumu la kila mwananchi ili kuweka afya za Wanadodoma salama.
Dkt. Leonard Subi (wa pili kulia) wakati akiongea na Waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma ikiwa ni siku ya matumizi ya choo Duniani na wiki ya usafi wa mazingira Tanzania.
Afisa Afya wa Jiji la Dodoma Abdallah Mahia alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa tovuti hii kuhusu hali ya Vyoo katika Jiji la Dodoma na sababu iliyosababisha Mkoa wa Dodoma kushika nafasi ambayo si nzuri kitaifa huku akiweka msisitizo kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kujenga vyoo bora kwa afya zao.
Chanzo: Wizara ya Afya (Instagram), tovuti ya Jiji Dodoma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.