Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeridhishwa na ujenzi unaoendelea wa kituo kipya cha afya katika Kata ya Nkuhungu na kusema kuwa Kamati ya Ujenzi imetimiza wajibu wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira, Jaffar Mwanyemba alipoongoza Kamati ya Fedha na Utawala ‘route one’ kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo kipya cha afya katika Kata ya Nkuhungu mwishoni mwa wiki.
Mwanyemba alisema kuwa wajumbe wameridhika na kazi nzuri iliyofanywa katika utekelezaji wa ujenzi wa majengo ya kituo hicho cha afya. Aidha, kamati zinazosimamia ujenzi huo zilipongezwa kwa kutimiza wajibu wake vizuri katika kusimamia taratibu za ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nkuhungu, Mwasiti Abdallah alisema kuwa ujenzi ulianza tarehe 17/3/2022 kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Lengo ni kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi baada ya kuwa na uhitaji wa huduma za afya katika kata na maeneo jirani. Jumla ya shilingi 207,996,246 zimepokelewa kwenye akaunti ya kata kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na maabara. Hadi sasa majengo ya wagonjwa wa nje na maabara yamepauliwa. Miundombinu ya maji na umeme imeshasambazwa na shughuli za ukamilishaji wa majengo unaendelea na umefikia asilimia 70 ya utekelezaji” alisema Abdallah.
Alisema kuwa kiasi cha fedha kilichotumika ni shilingi 187,000,000. Baada ya awamu hii itafuata ujenzi wa majengo ya upasuaji, wodi ya wazazi na kichomea taka, aliongeza.
Akiongelea faida za mradi, alisema kuwa ujenzi huo utakapokamilika utaisaidia jamii ya watu wapatao 38,622 kupata huduma za kliniki ya watoto karibu na jamii. Faida nyingine ni kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya katika kata ya nkuhungu kwa sababu kata hiyo haikuwa na kituo chochote cha serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.