MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezindua kauli mbiu ya Mkoa kwa mwaka 2024 yenye lengo la kutatua kero za wananchi wa Dodoma.
Kauli mbiu hiyo inayosema "kero yako, wajibu wangu" imezinduliwa wakati wa kikao cha Kamati ya ushauri wa Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Senyamule amesema uzinduzi wa kauli mbiu hiyo, ni utekelezaji wa agizo la Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kila kiongozi kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa eneo lake.
"Tumekuja na kauli mbiu hii ili kuleta hamasa kwa watumishi wa Serikali ngazi zote kuhakikisha kila Mtumishi anashughulika na kero za wananchi kwenye eneo lake. Maagizo yalisema kila Mtumishi atenge siku ya kusikiliza kero, Maafisa utumishi wote wasimamie utatuzi wa kero za wananchi. Kazi hii isiwe ya mtu mmoja". Alisisitiza Senyamule
Mbali na uzinduzi huo, kikao cha Kamati ya ushauri Mkoa, kimejikita zaidi kujadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Taasisi mbalimbali za umma kwa mwaka wa fedha 2023/24 sambamba na uwasilishaji wa mapendekezo ya bajeti ya 2024/25.
Mapendekezo ya bajeti mpya ni shilingi Bilioni 398 zinazojumuisha Bilioni 275 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 123 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile kugharamia miradi ya Halmashauri katika sekta za Elimu, afya , miradi ya kilimo, mazingira, n.k
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Mkoa, amefunga kikao hicho kwa kuomba bajeti hiyo upya iidhinishwe. Pia ametoa maagizo kadhaa yakiwemo kufuatiliwa watoto wote ambao hawajarudi shuleni mpaka Sasa, fedha za lishe zipelekwe kwenye Halmashauri na Maandalizi kwa ajili ya mashindano ya AFCON yaanze kufanyika kwani Dodoma itakua mwenyeji wa mashindano hayo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.