SERIKALI imetatua changamoto za uhaba wa miundombinu ya majengo katika Shule ya Sekondari ya Kibakwe wilayani Mpwapwa kwa kutoa Sh milioni 150 ili kujenga majengo na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia wanafunzi 1,280 wa shule hiyo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge aliyetembelea kukagua ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo hasa maktaba na bwalo la shule, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kibakwe, Sajigwa Nikupala aliishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo kwani zimesaidia kupunguza adha kwa wanafunzi hasa baada ya kuanza kutoa elimu ya kidato cha tano na sita kwa wasichana.
Nikupala aliipongeza Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuwapatia mradi huo mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia kuinua maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Awali shule hiyo mara baada ya kupandishwa hadi na kuwa na kidato cha tano hadi sita, ilkabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa, mabweni, maktaba na bwalo, lakini ilipofika Januari 18, mwaka jana, shule hiyo ilipokea fedha kutoka serikali kuu kupitia programu ya lipa kulingana na matokeo (EP4R) ambapo kati ya fedha hizo, sh milioni 100 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa bwalo na sh milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa maktaba.
“Ujenzi huo ulitumia mfumo wa 'force account' ambapo vifaa vilinunuliwa kufuatia mchanganuo ulioandaliwa na mhandisi wa ujenzi wa halmashauri na kazi ya ufundi ilifanywa na fundi aliyepatikana kwa ushindani,” alisema .
Aidha, Nikupala alisema, ujenzi wa maktaba umekamilika kwa asilimia 100 na imeanza kutumika, isipokuwa ujenzi wa bwalo kiasi cha fedha zilizotolewa hazikutosha, hivyo Juni 10, mwaka huu shule hiyo ilipata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpwapwa cha kutumia sh milioni 5.8
Alisema fedha hizo zilikuwa sehemu ya fedha zilizotolewa kupitia Mpango wa Elimu bila Malipo ambayo zilipokelewa shuleni hapo kipindi cha likizo cha Covid-19 na hivyo kufanya jumla kuu ya mradi huo kuwa sh milioni 105 na umekamilika kwa asilimia 80.
Nakupala alizidi kusema kuwa eneo lililobaki ni ujenzi wa jiko la nje na vyoo, na kutengeneza viti na meza ambavyo gharama yake inakadiriwa kuwa sh milioni 30.
Mkuu wa shule alisema, mafanikio ya mradi huo hasa bwalo la shule ni wanafunzi kupata eneo la kupatia chakula, kutumika kama ukumbi wa shughuli mbalimbali kielimu, kutumika kama chanzo cha mapato kwa shule na jamii imehamasika kusomesha watoto wao katika shule hiyo.
Pamoja na mafanikio haliyopatikana pia kulikuwa na changamoto zikiwemo za mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za vifaa vya ujenzi, usafirishaji wa vifaa kwa shida hasa kipindi cha masika na fedha inayotolewa kutotosheleza kulingana na uhalisia wa mradi.
Akizungumza mara baada ya kusikia ripoti hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri ya kuelimisha wanafunzi kwani wao ndio wanaotegemewa katika nafasi ya kwanza kufuta ujinga wa watoto hao hasa kama vitabu na mabweni yatakuwapo.
Aliwasihi kwamba waendelee kuwa wastahilimivu katika kutoa elimu na kuelimisha watoto ili wapate elimu bora kwa ajili ya manufaa yao na faida ya taifa zima ili kuja kusimamia raslimali za umma.
Aliwaagiza viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, mara wanapopanga bajeti basi wasisahau sekondari ya Kibakwe kwa ajili ya kupata fedha sh 30,000 kwa ajili ya kujenga jiko na vyoo kwa ajili ya matumizi ya bwalo la sekondari.
Alisema ujenzi wa bwalo hilo ni uwekezaji muhimu kwani litatumika katika kazi nyingi zikiwemo za kulia chakula, kufanyia mitihani pamoja na mikutano mbalimbali.
Akizungumza na wanafunzi, Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge aliwataka waendelee kusoma kwani Tanzania itaendelea kuwapo na kwa kusoma huko wajue ajira zipo na taifa hili linawategemea kushika madaraka baada ya waliopo kustaafu.
Shule ya Sekondari Kibakwe ambayo ni miongoni mwa shule 24 za sekondari katika wilaya ya Mpwapwa, ilianzishwa mwaka 1990 kama shule ya kutwa ya wasichana na wavulana, lakini mwaka 2015 ilipandishwa hadhi kuwa ya kidato cha tano na sita kwa wasichana pekee.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1280 wakiwemo wavulana 511 na wasichana 769, kati ya hao wasichana wa kidato cha tano na sita ni 210 ambao wanasoma michepuo ya HGL, HGK na CBG.
Akizungumza mwalimu wa Taaluma, Asalu Matamla alisema, shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani yake ya kidato cha sita, mwaka jana wanafunzi waliopata daraja la kwanza walikuwa 20, la pili 63, daraja la tatu 28, na hakuwa na waliopata daraja la nne wala sifuri.
Naye Mwalimu wa Masomo ya Fizikia na Hesabu, Nurdin Lundakris alisema matokeo mazuri ya wanafunzi hayo yanatokana na juhudi zao
Jengo ambalo ni Bwalo la Shule ya Sekondari Kibakwe.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibakwe wakimsikliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (hayupo pichani) alipotembelea shule hiyo jana.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.