MBUNIFU Kessy Mohamed amebuni kifaa wezeshi kwa watu wenye ulemavu wa miguu yote kuweza kuendesha gari “disable driving mechanism” (DDM) kwa lengo la kuwasaidia watu hao kuweza kuendelea na majukumu yao baada ya kupata ulemavu.
Mohamed aliyasema hayo wakati akielezea ufanisi wa kifaa hicho katika banda la Taifa innovations lililopo katika maonesho ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mohamed alisema “nilifikiria kubuni kifaa wezeshi kwa watu wenye ulemavu wa miguu yote kuweza kuendesha gari kwa sababu mimi ni dereva na ndiyo kazi yangu. Hivyo, baada ya kupata changamoto ya ajali nilipopona majeraha yangu na ugumu wa maisha niliokuwa nao ndiyo wazo la kurudi barabarani lilipoanza na ndio wazo la kifaa wezeshi lilipoibuliwa” alisema Mohamed.
Mohamed alisema kuwa ubunifu wa kifaa hicho wezeshi ulianza mwaka 2015 na mbunifu wa kwanza alikuwa Joseph Sanga. “Kwa miaka mitano sasa ni mimi pekee ndiyo natumia kifaa hiki. Ni kwa sababu mamlaka za serikali wamekuwa wazito kupitisha kifaa hiki kiwe rasmi. Kwa kipindi chote, kifaa hiki ni salama na hakina shida yoyote wakati wa uendeshaji” alisema Mohamed.
Mbunifu huyo, alisema kuwa mtu yoyote anaweza kuwa mlemavu na kusisitiza kuwa ni jambo la kawaida katika uumbaji wa mungu na kushauri kutumia akili kubadilisha fikra za kuwa ulemavu ni kushindwa. Mtu mwenye ulemavu anaweza kubuni jambo ambalo litaweza kusaidia wengi.
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendesha Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa madhumuni ya kutambua, kuadhimisha, kujenga, kukuza na kuendeleza ubunifu wa watanzania katika nyanja za sayansi na teknolojia ili kuchangia juhudi za kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.