Na. Nancy Kivuyo, MATUMBULU
MIKOPO isiyo na riba ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imekuwa chachu ya kusukuma maendeleo katika sekta za kilimo, ufugaji na ujasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kikundi hicho kufuatilia manufaa ya mikopo hiyo kwa jamii, Mwenyekiti wa Kikundi cha Kilasara, Judika Urio alisema kuwa wanawake hao wamenufaika na mkopo huo usio na riba. “Kikundi chetu tupo watano, tulipata takribani shilingi milioni 20 ambazo tuliwekeza katika ufugaji wa kuku, bata mzinga, bata bukini na sungura. Baada ya mafanikio ya ufugaji huo, tulipata faida ambayo ilituwezesha kuanzisha mradi mwingine wa uzalishaji wa samaki kama mnavyoona kwenye mabwawa haya, tumeweka mbegu ya samaki wapatao elfu 10 ambao tunategemea baada ya mwaka ndio tuvune” alisema Urio.
Alimshukuru Rais, kwa kuyajali makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kusema kuwa amewainua na kuwapa kipaumbele. “Namshukuru pia mbunge wetu, Anthony Mavunde na Diwani, Emmanuel Chibago, tunaamini wana mchango mkubwa katika kuishauri serikali kuangalia makundi haya katika jamii ili yawezeshwe kujikwamua kiuchumi” alimalizia Urio.
Nae, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Matumbulu, Merina Gombo, alisema kuwa wanasaidia makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata elimu sahihi juu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na kuwasimamia. “Lengo letu ni kuhakikisha makundi haya yanapata mikopo ya asilimia 10 ili kujikwamua kiuchumi. Yapo makundi nane yaliyopata mikopo hiyo ikiwemo kikundi hiki cha Kilasara ambao ni mfano wa kuigwa na akina mama wengine wanaotaka kuja kukopa na kujiingiza katika shughuli za maendeleo” alisema Gombo.
Kwa upande mwingine, mnufaika wa ajira kupitia Kikundi cha Kilasara, Furaha Anthony alisema kuwa anakishukuru kikundi hicho kwa kumpatia ajira. “Ninafuga hawa samaki katika haya mabwawa tangu mradi huu umeanzishwa. Hawa samaki wanakuwa kwa muda wa miezi nane hadi mwaka ndio tunawavuna. Kwahiyo, ni mradi mzuri unatunufaisha sisi wakazi wa Mtaa wa Nyerere” alisema Anthony.
Kata ya Matumbulu ina jumla ya wakazi takribani 11,169, wakijishughulisha na kilimo cha zabibu, ufugaji wa ng’ombe na kilimo cha kisasa cha mbogamboga na matunda.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.