Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MWENYEKITI wa kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, Johnick Risasi ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata mikopo ya asilimia mbili kutoka mapato ya ndani.
Meja Mst. Risasi alitoa pongezi hizo alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Dodoma kutembelea kikundi cha watu wenye ulemavu cha TUJIKUBALI kilichopo Mtaa wa Nzuguni ‘B’ Kata ya Nzuguni, jijini Dodoma.
Meja Mst. Risasi alisema kuwa kitendo cha Halmashauri kuwakopesha watu wenye ulemavu ni kuonesha kuwajali watu hao. “Mheshimiwa Rais Samia anazungumzia usawa kwa watu wote. Watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kujiletea maendeleo. Ushauri, watu hawa watafutiwe sehemu nzuri na kuangalia jinsi ya kuwezeshwa kulipa pango. Huku wanapofanyia shughuli zao pamejificha sana” alisema Meja Mst. Risasi.
Mwenyekiti huyo alishauri viatu wanavyoshona viboreshwe zaidi kwenye umaliziaji ili kuwa na muonekano mzuri na wa kuvutia zaidi. “Nimefurahi sana kwa juhudi hizi. Uongozi wa Kata uwasaidie kufikia masoko na ikibidi wasaidiwe kupata Bajaji kwa ajili ya kurahisisha usafiri wao” alisisitiza Meja Mst. Risasi.
Akisoma taarifa fupi ya kikundi cha Tujikubali walemavu, Mweka Hazina, Pauleta Lesso (pichani juu) alisema kuwa miundombinu na usafiri ni changamoto. “Miundombinu na usafiri kwa sisi walemavu ni changamoto kubwa hasa wakati wa kutafuta masoko na kuuzia bidhaa zetu. Vile vile, uhaba wa masoko ya kuuzia viatu baada ya kutengeneza pia ni changamoto kwetu” alisema Lesso. Aidha, aliongeza kuwa kutawanyika kwa baadhi ya wanakikundi kutokana na sababu binafsi kumepelekea kupoteza uaminifu katika kikundi, aliongeza.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rukia Bakari alisema kuwa halmashauri imepanga kujenga jengo kwa ajili ya shughuli za wajasiriamali eneo la Nzuguni. “Jengo hilo likikamilika litawawezesha wajasiriamali kuwa sehemu moja na inayofikika kirahisi kwa ajili ya kuuza bidhaa zao” alisema Bakari.
Nae Diwani kwa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega alisema kuwa kikundi chicho kinakabiliwa na changamoto ya usafiri. “Tumeshawaombea usafiri kwenye mfuko wa Jimbo na bahati nzuri mheshimiwa Mbunge amelipokea vizuri. Mbunge ameahidi kuangalia katika bajeti yake kuona jinsi ya utekelezaji wake” alisema Luhega.
Mwenyekiti wa kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi akiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na kikundi cha Tujikubali walemavu kilichopo kata ya Nzuguni Jijini Dodoma.
Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na kikundi cha Tujikubali walemavu kilichopo Kata ya Nzuguni ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 2 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.