KATIKA kuonesha kuwa imedhamiria kuwakwamua vijana kiuchumi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekikopesha kikundi cha vijana wajasiriamali cha Umapido kilichopo kata ya Viwandani jijini humo shilingi Milioni 300.5 na tayari kikundi hicho kimeanza kufanya marejesho ya mkopo huo.
Kikundi hiki kinachojishughulisha na usafirishaji wa abiria kimeajiri vijana zaidi ya 67 ambao ni madereva wa vyomba vya kusafirisha abiria na mizigo ambapo kilipata mkopo huo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana mwaka 2020.
Taarifa ya kikundi hicho mbele ya Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri hiyo iliyowatembelea kukagua shughuli zao leo Oktoba 12, 2021 inaonyesha kuwa, baada ya kupata mkopo huo, kikundi kilinunua vyombo vya usafirishaji abiria ikiwemo bajaji na pikipiki pamoja na guta kwa ajili ya kusafirishia mizigo.
“Baada ya kupata fedha hizo kikundi kilinunua bajaji 20, pikipiki maarufu kama bodaboda 46, pamoja na guta moja kwa ajili ya kusafirishia mizigo” ilisema sehemu ya taarifa ya kikundi hicho.
Taarifa hiyo ilisema kwa sasa kikundi hicho kinafanya marejesho ya zaidi ya shilingi milioni 12 kila mwezi na tayari kimesharejesha zaidi ya milioni 100.24 kwa Halmashauri ya Jiji hilo.
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Emmanuel Chibago walikipongeza kikundi hicho na kutoa wito kwa vikundi na vijana mmoja mmoja kujifunza kwa kikundi hicho kilichoonyesha mafanikio.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.