WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Maafisa Mazingira wa Mikoa nchini kuhakikisha wanasimamia Halmashauri zilizopo katika Mikoa yao kupanda miti milioni moja na laki tano kila mwaka ili kuhifadhi mazingira kwa vizazi vya sasa na baadaye.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo jana Jijini Dodoma wakati akizindua jiwe la utambulisho eneo la Msitu wa Jiji Medeli Jijini hapa .
‘'lakini isiishie tu katika kupanda miti, kama Dodoma walivyotuambia miti imekuwa kwa asilimia 88% na mimi nikienda katika mkoa, moja ya taarifa ninayotaka kuipata mmpenda miti mingapi katika kila halmashauri, mingapi imeota na Dodoma Wamefanya vizuri’’ Waziri Ummy amesema
Wakati huo huo Waziri Ummy amezitaka Taasisi binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Halmashauri katika kuhakikisha miti hiyo milioni 1.5 inapandwa kila mwaka huku akisema kuwa wanakuja na mpango kabambe wa kuboresha mazingira katika majiji sita.
‘’Majiji hayo ni Dodoma, Tanga, Mwanza, Arusha, Dar es salaam na Mbeya. Tunataka kuonesha kwamba unaweza kuwa katika halmashauri ya jiji na bado tukapanda miti, tukawa na misitu ya jiji na mipango safi ya uhifadhi ya majitaka lakini pia masuala ya usimamizi wa taka ngumu’’ amefafanua Waziri.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Mazingira Dkt. Severin Kalonga wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyapori (WWF) amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais walibuni mradi wa kuunga mkono juhudi za serikali za kukijanisha Dodoma ikiwa ni pamoja na juhudi za kupanda miti hapa nchini.
Naye Afisa Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Zuirekha Kashwamba amesema TFS imejitahidi kupanda miti, kwani toka kampeni ya Dodoma ya kijani imeanza wamefanikiwa kupanda miti Milioni moja na laki nane ambapo kwa sasa wanamiche laki tano ndani ya bustani zao ambayo inasubiriwa kupandwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.