KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim ameipongeza serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo elimu nchini.
Pongezi hizo alizitoa alipoongoza Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kutembelea, kukagua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Dodoma English Medium katika Kata ya Ipagala jijini Dodoma.
Kaim alisema “niipongeze serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayofanya ikiwa ni pamoja na kutenga na kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo. Tumejiridhisha na nyaraka za mradi huu baada ya kuzikagua zipo vizuri sambamba na mradi nikiri mpaka hatua hii kazi kubwa na nzuri imefanyika. Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 tumeridhia uwekaji jiwe la msingi” alisema Kaim.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Dodoma English medium kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alisema kuwa lengo la kujenga shule hiyo ni kutoa elimu bora zaidi ambayo itasaidia kupata wataalam mbalimbali kwa maendeleo ya kiuchumi. “Lengo lingine ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na msingi na kuwezesha wananchi wa kipato cha kati kupata fursa ya kuwapeleka watoto katika shule ya mchepuo wa kiingereza inayomilikiwa na Serikali” alisema Myalla.
Alisema kuwa halmashauri ilipokea shilingi 400,000,000 tarehe 20 Aprili, 2023 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya awali na msingi. Halmashauri ya Jiji Dodoma imetoa shilingi 58,316,799 kupitia mapato ya ndani kusaidia ujenzi huo. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, utekelezaji wa mradi huu ulianza rasmi tarehe 05.05.2023. Tumefanikiwa kujenga Jengo la Utawala, vyumba 11 vya madarasa, ikiwa madarasa 02 ni kwa ajili ya Elimu ya Awali na madarasa 9 kwa ajili ya darasa la I hadi la VII. Aidha, yamejengwa matundu 38 ya vyoo, matundu 6 ni kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya Awali na 32 kwa ajili ya elimu ya msingi. Hadi sasa mradi upo hatua za umaliziaji. Miti 200 imepandwa kati ya hiyo, Miti 100 ni ya matunda na Miti 100 ni kwa ajili ya kivuli” alisema Myalla.
Akiongelea gharama za mradi huo, alisema kuwa umetumia shilingi 330,882,100 na unatarajia kukamilika tarehe 31 Oktoba, 2023.
Kuhusu mafanikio ya mradi, alisema kuwa utatoa huduma ya elimu ya mchepuo wa kiingereza na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zenye upungufu wa vyumba vya madarasa. “Mafanikio mengine ni kuleta huduma ya elimu karibu na jamii, kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika suala zima la kitaaluma kutoka asilimia 89.9 kwa mwaka 2022 na kufikia asilimia 100 na kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti” alisema Myalla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.