Na.Sifa Stanley, DODOMA
KIONGOZI wa mbio za mwenge kitaifa, Sahili Geraruma ampongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru kwa kutekeleza agizo la Serikali kutoa mikopo kwa vijana, kinamama pamoja na walemavu.
Pongezi hizo alizitoa katika mbio za Mwenge wa Uhuru ulipotembelea mradi wa kikundi cha vijana cha Kiu ya Ufanisi kilichopo Nanenane Kata ya Nzuguni, kinachojishughulisha na kilimo cha nyanya kwa njia ya kisasa.
Kiongozi huyo alisema kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma anafanya vizuri kwa kufanya utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan, kuwa halmashauri zitoe mikopo kwa vijana, watu wenye ulemavu pamoja na kinamama.
“Mwenge wa Uhuru unatoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, kwa kutekeleza moja ya maagizo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa mikopo kwa vijana, kinamama, pamoja na watu wenye ulemavu. Mkurugenzi mtu akija kuomba mkopo kama ametimiza vigezo mpatie mkopo,” alisema Geraruma.
Aidha, aliwaagiza wanufaika wa mikopo inayotolewa na jiji kuwa waaminifu katika kurejesha mikopo yao na warejeshe mikopo hiyo kwa wakati ili mikopo izidi kuwanufaisha watu wengine.
“Wanufaika wa mikopo hii, hakikisheni kuwa mnarejesha mikopo kwa wakati ili muendelee kuaminika na kukopesheka zaidi, lakini pia mtatoa nafasi kwa watu wengine kunufaika na mikopo hii isiyo riba”,alisema Geraruma.
Sambamba na hilo, alitoa wito kwa watu wote kujitokeza kuchukua mikopo yao ambayo wataitumia kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kuwasaidia wanufaika wa mkopo kujikwamua kiuchumi na kulisaidia taifa kusogeza mbele gurudumu la maendeleo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Dodoma zimefanyika Tarehe 17/08/2022 ambapo ulikimbia umbali wa jumla ya kilomita 129.5, na ukiwa katika wilaya hiyo ulitembelea, kukagua pamoja na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendeshwa ndani ya jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.