Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2022 Sahili Geraruma amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza agizo la Rais kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Pongezi hizo alizitoa baada ya kutembelea mradi wa kilimo wa kikundi cha Kiu ya Ufanisi na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Geraruma alisema kuwa Halmashauri ya Jiji inakopesha fedha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Alishauri kuwa fedha hizo zinazokopeshwa kwa vikundi zitumike kufanya shughuli za maendeleo.
“Nimpongeze Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa halmashauri kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo. Nitoe rai kwamba watanzania wote wenye sifa watakaokuja kukopa wapewe mikopo” alisema Gararuma.
Aidha, aliwataka wakopaji wa mikopo hiyo kuirejesha kwa wakati ili wakopaji wengine waweze kupata fursa ya kukopa. “Mimi nimependezwa na kazi inayofanywa na vijana wenzangu, endeleeni kwa mujibu wa malengo mliyojiwekea” alisema Geraruma.
Akisoma taarifa ya mradi wa kilimo wa kikundi cha Kiu ya Ufanisi kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022, Mwenyekiti wa kikundi, Onesmo Mnyamagola alisema kuwa kikundi hicho kilikopa ili kuwezesha wanakikundi kujiajiri na kuweza kuendesha maisha yao na kununua vitendea kazi.
Alisema kuwa mradi huo ulinunua kitalu nyumba kwa shilingi 14,234,000.00. Vitu vingine vilivyonunuliwa ni “pampu shilingi 5,500,000.00 kusafisha kisima kwa shilingi 1,200,000.00, ununuzi bomba za maji za plastiki (PVC pipe) rola moja shilingi 850,000.00, ununuzi wa nyaya za kupeleka umeme kwenye pampu mita 200 shilingi 2,400,000.00 ununuzi wa mfumo wa umwagiliaji shilingi 3,527,000.00, ununuzi wa pembejeo kama mbolea, mbegu, kamba za kufungia nyanya na viuatilifu shilingi 2,020,000.00, ununuzi wa miti shilingi 3,250,000.00, ununuzi wa samadi shilingi 600,000.00, chombo cha usafiri shilingi 3,050,000.00 na ununuzi wa vitendea kazi shilingi 1,200,000.00” alisema Mnyamagola.
Alisema kuwa baada ya kupata mkopo wamefanikia mambo kadhaa. “Kupitia mkopo huu tumefanikiwa kukamilisha lengo kuu la kutengeneza kitalu nyumba, kufunga mifumo ya umwagiliaji pamoja na kuajiri vijana watatu katika shughuli za mradi na kuongeza mapato ndani ya Serikali kwa kulipa kodi kupitia manunuzi mbalimbali” Mnyamagola.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.