KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim amefurahishwa na mamia ya wananchi wa Kata ya Nzuguni waliojitokeza kwa wingi kuupokea na kuushangilia Mwenge wa Uhuru ulipofika kuweka jiwe la msingi mradi wa Barabara ya Nzuguni-Mahomanyika.
Kaim alisema “kabla sijatoa majumuisho ya Mwenge wa Uhuru kukagua barabara hii niwapongeze wananchi wa Nzuguni kwa namna mlivyojitokeza kwa wingi, haya ni mafuriko makubwa, shamrashamra na vibe la kutosha kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru. Hakika ninyi ni watu wema na wazalendo wakubwa”.
Aidha, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma, Anthony Mavunde kwa hamasa yake katika Mwenge wa Uhuru. “Pongezi kwa Mheshimiwa Mavunde tunakushukuru kwa kazi nzuri pamoja na wingi wa majukumu uliyonayo lakini umeona umuhimu wa kujumuika nasi. Hongera sana Mungu akubariki wewe ni mtu bingwa” alisema Kaim.
Akiongelea mradi wa Barabara ya Nzuguni-Mahomanyika kilometa tano alisema kuwa imejengwa kwa kiwango bora. “Mbio za Mwenge wa Uhuru tumepokea taarifa ya mradi na Mwenge wa Uhuru umefanya ukaguzi wa nyaraka mbalimbali na kukagua hatua ya ujenzi wa mradi iliyofikiwa. Mhe Mkuu wa Wilaya ukaguzi wa kina umefanywa na Mwenge wa Uhuru umejiridhisha nyaraka zote zipo vizuri, vigezo na ubora umeonekana. Hongera sana Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini. Mwenge wa Uhuru 2023 umeridhia uwekaji wa jiwe la msingi mradi huu” alisema Kaim.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Barabara ya Nzuguni-Mahomanyika Kilometa tano kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Dodoma, Mhandisi Emmanuel Mfinanga alisema kuwa barabara hiyo imejengwa kwa lami ngumu. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023; Barabara ya Nzuguni- Mahomanyika ina Kilometa 13 kutoka Nzuguni hadi kufika Barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer Ring road). Kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilitenga fedha shilingi 6,109,748,702 kwa ajili ya ujenzi wa Kilometa tano za lami ngumu” alisema Mhandisi Mfinanga.
Akiongelea lengo la ujenzi wa barabara hiyo alisema kuwa utasaidia kupunguza msongamano kwenye barabara kuu iendayo Morogoro. “Lengo lingine ni kupunguza mafuriko, kuwezesha shughuli za Zimamoto, Mradi wa Maji Safi kufikika kiurahisi na kupanua mtandao wa barabara kwa kuunganisha barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer ring Road)” alisema Mhandisi Mfinanga.
Alisema kuwa mradi huo ni wa manufaa kwa wananchi. ”Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, kukamilika kwa mradi huu kutawezesha shughuli za kijamii kufikika kirahisi kwasababu barabara hii ni kiungo kikubwa kwenda Mji wa Serikali (Mtumba), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Kituo kikuu cha Mabasi Dodoma na Soko kuu la Job Ndugai lakini pia wananchi wa Kata ya Nzuguni wapatao 50,454, kufika katika maeneo yao kirahisi. Pia uwepo wa barabara utawezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika na hivyo kukuza uchumi wa jamii na Taifa” alisema.
Gharama za mradi huo ni shilingi 6,109,748,702, na shilingi 5,246,805,322 sawa na asilimia 86 kimelipwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.