Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2022 Sahili Geraruma ameridhishwa na wingi wa wananchi waliojitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru wilayani Dodoma na kushiriki mkesha uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Chang’ombe kuwa wameutendea haki Mwenge wa Uhuru.
Kauli hiyo aliitoa katika uwanja wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru uliofanyika katika shule ya msingi Chang’ombe iliyopo Kata ya Chang’ombe jijini hapa.
Geraruma alisema kuwa wingi wa watu waliojitokeza ni ishara ya kuheshimu na kuunga mkono Mwenge wa Uhuru. Aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya kupokelea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru na mkesha. “Pongezi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri. Tunatamani kuendelea kubaki hapa Jiji la Dodoma lakini kwa majukumu na itifaki ya Mwenge wa Uhuru tunalazimika kuondoka” alisema Geraruma.
Akiongelea Sensa ya watu na makazi, alisema kuwa sensa hiyo ni muhimu kwa wote. “Sensa ya watu na makazi ni zoezi muhimu kwa mustakabari wa wananchi wetu na maendeleo ya nchi kwa ujumla” alisema Geraruma.
Awali akimkaribisha Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kuaga mamia ya wananchi waliojitokeza katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru 2022, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema kuwa wingi na mafanikio hayo ni kutokana na ushirikiano. “Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, napenda kumshukuru Diwani wa Kata ya Chang’ombe na madiwani wote wa Jiji la Dodoma wakiongozwa Mstahiki Meya Prof. Davis Mwamfupe, Mkurugenzi wa Jiji na wakuu wa Idara na wananchi wote na kwa uzito huohuo, viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma kushiriki vema katika mbio za Mwenge wa uhuru 2022. Pongezi wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa, mkoa na wilaya. Umoja na mshikamano ndiyo msingi wa maendeleo” alisema Shekimweri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.