SERIKALI imesema Vijana ni kundi tegemewa kwa Taifa kwani wanabeba dira ya Taifa kutokana na mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya changamoto zinazowakabili zikiwemo za UKIMWI na vitendo vya ukatili.
Hayo yamesemwa leo Septemba 11, 2021 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Ummy Nderiananga wakati akizindua Programu ya ONGEA Kitaifa Jijini Dodoma yenye lengo kuwafikia Vijana nchi nzima kuwapa uelewa wa masuala ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia vyombo vya habari.
Katika uzinduzi wa programu hiyo TACAIDS inashirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) ambapo katika programu hiyo kumetengenezwa vipindi maalum vya redio vyenye ujumbe unaowalenga vijana kwa kutumia lugha yao na mzingira yao ili kuwezesha kundi hilo kutambua masuala VVU na Ukimwi kupitia vipindi vitakavyorushwa na Clouds FM na East Africa Radio.
Naibu Waziri Ummy alieleza kuwa Uzinduzi wa programu ya kimataifa ya ONGEA ni fursa ya kuwafikia vijana balehe nchini kupitia vyombo vya Habari ili kuwaongezea uelewa kuhusu matatizo na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku ikiwemo maambukizi ya VVU ili wachukue hatua za kuandaa mikakati mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hizo.
“Serikali kupitia uongozi wa Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan tunaamini vijana ndio waliobeba taifa letu na ndiyo nguvukazi ya nchi kwa hiyo kwa pamoja lazima tuhakikishe ushirikiano unakuwepo katika kulinda afya zao,” amesema Naibu Waziri Ummy.
Aidha, Ummy ametoa wito kwa Vijana nchini wafuatilie maudhui ya programu hiyo ya ONGEA kwa kina huku akifafanua kuwa programu hiyo itakuwa ya miezi tisa lengo likiwa kuwafikia Vijana na walezi wao ili waweze kuondoa vikwazo kwa Vijana balehe kupitia vipindi vya redio.
“Kupitia programu hii tufanikiwa kuongeza uelewa pamoja na ongezeko la upimaji wa afya kutoka asilimia 43 mpaka 57 hivyo kutakuwa na manufaa makubwa, “ amesisitiza Naibu Ummy.
Pia amewataka wazazi kuwajibika na kuvunja ukimya kwa kutenga muda wa kuongea na Watoto wao, kuwapa elimu ya afya na uzazi ili kuepuka mazingira hatarishi huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia Vijana watimize ndoto zao.
“Nitoe wito kwa wazazi tuongee na watoto wetu, kwa kufanya hivyo tutasikia mengi kutoka kwao na kujua mahitaji yao muhimu katika kuwasaidia waepuke vishawishi, ni matumaini yangu programu hii inakuza uhusiano baina yao na huduma za afya na pia kuwajengea uhuru wa kujitokeza kupima afya zao,” amefafanua.
Katika hatua nyingine ameyapongeza Mashirika mabalimbali na wadau kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania akisema Serikali itaendelea kufanya Kazi pamoja nao katika kusimamia ustawi wa Vijana huku akisisitiza vyombo vya habari kushiriki kikamilifu kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi.
“Kipekee niwapongeze TACAIDS na wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) kwa kuhakikisha tunashirikiana katika kutekeleza kwa pamoja programu hii ya ONGEA ili vijana waweze kuongea na kufundishana na kupeana mipango ya kujilinda na kuwa wenye afya njema na kuonyesha mchango wao katika kutambuliwa mchango wao kwenye taifa,” amefafanua zaidi.
Sambamba na hayo alihimiza programu hiyo kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanashirikishwa kwa karibu kulingana na aina ya ulemavu walionao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri ameeleza kuwa Vijana wengi hushiriki ngono katika umri mdogo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na elimu rika na kufanyiwa ukatili wa kingono na watu wao wa karibu vitendo vinavyochangia kuongezeka kwa maambukizi ya VVU.
“Kuna sababu nyingi zinazochangia maambukizi mapya zikiwemo mila potofu, tamaa za wazazi, kuruhusu watoto kulala na wageni bila kuwafahamu vizuri. Shekimweli amesema kuna watu 98,000 wenye umri kati ya miaka 10-19 wanaishi na VVU hivyo wazazi lazima tuwajibike na kutoa nafasi watoto wasikilize vipindi hivi na kutoa maoni yao maana ndiyo wahusika,” ameeleza Shekimweri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko amesema kwa katika maambukizi mapya ya Ukimwi asilimia 40 ni kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24 ambapo kwa mwaka 2017 maambukizi yalifika 72,000 yakijumuisha Watoto, Vijana na Wazee.
“Kutokana na takwimu hizi TACAIDS tuliona umuhimu wa kutoa elimu kwa umma hususan vijana na tulipokea maelekezo ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Mgahama katika kufikisha elimu kwa vijana na haya ndio matokeo ya kuanzishwa kwa programu hiyo,” amesema Dkt. Maboko.
Vile vile, Kaimu Mwakilishi Mkazi kutoka UNICEF, Daniel Baheta ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuhakikisha Vijana wanakuwa na ustawi na kuwa sehemu ya maendeleo kwa Taifa lao.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu, Devotha Gabriel akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu alishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) na TACAIDS kwa kuanzisha mradi huo utakaoleta tija kwa vijana na Taifa katika kutokomeza janga hilo la ugojwa wa UKIMWI.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.