WATAALAM wamesema aina mpya ya virusi vya korona ‘double mutant’, ambavyo vimeonekana nchini India ni hatari zaidi kutokana na uwezo wake wa kubadilika mara kwa mara.
Kirusi hicho kipya aina ya B.1.617 ndicho kinaelezwa kuwa wimbi la pili kuipiga India, ambayo imeshuhudia maambukizi kufikia zaidi ya milioni 21 huku vifo vikifikia 230,168 hadi kufikia jana mchana.
Mtaalam wa maikobaolojia na virusi kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), Dkt. Joe Manyai amesema aina hiyo ya kirusi kina tabia ya kujibadilisha mara kwa mara.
“Kirusi hicho hicho kinajibadilisha kidogo kinachukua chembechembe nyingine ya jeni (gene) inatengeneza rangi nyeupe kidogo au hufifia na hujiweka kwa binadamu au mnyama.
Kina tabia ya kutumia protini, kinajibadilisha kidogo ili kuwa orijino, kinajibadilisha mara mbili, kama kilikuwa A kinabadilika kuwa B halafu baadaye kinakuwa C, kikifanya mabadiliko kinakuwa kirusi kingine ili kiweze kuenea kwa urahisi zaidi,” alisema Dkt. Manyahi.
Wakati wanasayansi wakiwa katika uchunguzi kuhusu aina mpya ya kirusi cha Korona kinachoua nchini India, wataalam wa afya nchini wametoa angalizo huku wakijata mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuepukana na kirusi hicho.
Madaktari wameiomba Serikali kupunguza mwingiliano wa watu, kuongeza upimaji na pia taasisi zenye uwezo ziruhusiwe kupima na nchi iandae hospitali za dharura zenye oksijeni za kutoka. Wameonya kuwa Tanzania inapaswa kuwa makini na kupata fundisho kutokana na wimbi la Korona nchini India.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na yanayoambukiza kutoka Hospitali ya Aga Khan, Mandela Makalala alisema virusi vya Korona vinabadilika badilika sana na vinaweza kuwa hatari zaidi ya tunavyofikiria kwa kuongezeka uwezo wa kusambaa zaidi na makali ya ugonjwa.
Alisema yatupasa kujitathmini kama nchi tumejiandaa vipi kupambana na wimbi la Korona litakalokuja.
“Madaktari tulio wengi tunadhani ni muhimu kuanza kutoa chanjo kwa makundi yaliyo katika hatari kubwa, yaani watumishi wa afya, wazee na wagonjwa wenye matatizo ya kiafya kama sukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na uzito kupita kiasi” alisema Dkt. Makalala.
Dkt. Makalala alisema ni muhimu kupunguza mwingiliano wa watu katika nchi ambazo zina wagonjwa wengi wa Korona na sisi Tanzania kama nchi tunahitaji kuongeza upimaji wa virusi vya Korona, kwa sasa ni maabala ya Taifa inayopita virusi hivyo.
“Turuhusu taasisi binafsi zenye uwezo wa kupima, hii itaongeza kasi ya kutambua maambukizi mapema na hivyo kuyapunguza. Inasikitisha na kuumiza moyo unapomwambia mgonjwa hospitali imejaa. Hili lilitokea katika awamu (wave) zote mbili za Korona hapa Tanzania, tusingelipenda kuliona tena” alisema Daktari huyo.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.