Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza uamuzi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuwa lugha ya Kiswahili inakuwa lugha rasmi ya 4 ya SADC kuanzia leo tarehe 18 Agosti, 2019.
Mhe. Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akifunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika kwa siku 2 (tarehe 17-18 Agosti, 2019) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.
TANZANIA imekabidhiwa rasmi uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) huku ikijivunia lugha yake ya Taifa, Kiswahili kupitishwa rasmi kuwa moja ya lugha itakayotumika katika shughuli rasmi za jumuiya hiyo.
Awali, Kiswahili kilitangazwa rasmi kuwa lugha ya nne ya jumuiya hiyo Dar es Salaam jana na aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC ambaye pia ni Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob alipohutubia Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo kabla ya kukabidhi madaraka kwa Mwenyekiti mpya, Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli.
Ni faraja kwa Watanzania wote kwa kuwa, ndiyo lugha ya Taifa lao. Ni kutakana na sababu hiyo, muda mfupi kabla ya kukabidhi madaraka kwa Rais Magufuli kuelekea hitimisho la hotuba yake, iliufanya ukumbi kulipuka kwa vigelele na shangwe hasa kutoka kwa wananchi wa Tanzania waliokuwa wengi kutokana na kuwa wenyeji wa mkutano.
Nchi 16 zinazounda SADC zimekuwa zikitumia lugha tatu ambazo ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa, hivyo kurasmisha lugha ya Kiswahili, kunaifanya jumuiya hiyo kuwa na lugha nne.
Watanzania, mbali na kujivunia kushika kijiti cha uenyekiti kwa kipindi cha mwaka mzima, lakini pia inatia faraja kubwa kuona lugha ya Kiswahili imepata nafasi hiyo kubwa na ni kati ya vipaumbele ambavyo Serikali imeviainisha wakati ikichukua kijiti hicho.
Ndiyo maana baada ya kutangazwa, hali katika Ukumbi wa Selous wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ikabadilika huku baadhi ya washiriki wa ufunguzi huo wakishangilia kwa kusimama na kuungwa mkono na watu wengi (wasio Watanzania) waliohudhuria tukio hilo.
Pia kwa msisitizo wa furaha hiyo, Rais Magufuli akajikuta mbali na kuanza kuzungumza kwa lugha ya Kingereza iliyozoeleka, akimalizia hotuba yake kwa lugha ya Kiswahili, kwanza kama Rais wa nchi inayozungumza lugha hiyo, hivyo kufunga pazia rasmi, lakini pili kama mwenyekiti mpya ambaye angependa kuona lugha hiyo inaanza kwa kasi ikianzia pake alipokabidhiwa kijiti jana.
Kama alivyosema Rais Magufuli, lugha ya Kishwahili ina historia yake katika jumuiya ya baadhi ya nchi za SADC, moja ikiwa ni jinsi ilivyotumika kama lugha ya ukombozi wakati wa harakati za kutafuta uhuru kwa nchi nyingi za Afrika.
Dk Magufuli akasema wakati akikabidhiwa kijiti hicho kuwa mapambano ya ukombozi wa Afrika yalifanikiwa na nchi zote za Afrika katika miaka ya 1990 zilipata uhuru moja ya sababu ikiwa ni matumizi ya Kiswahili.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Kiswahili ni lugha ya 10 duniani kuzungumzwa na watu wengi na ya 13 Afrika na ya sita katika nchi za SADC.
Akasema ni lugha rasmi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ni lugha rasmi kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Ikumbukwe kwamba Rais Magufuli pia alipofungua Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda, alitoa hutuba yake kwa Kiswahili kudhihirisha umuhimu wa lugha hiyo iliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika kwa ukombozi. Kufikia hapo, ni kazi kubwa imefanyika.
Pongezi ziwaendee pia wanaounda Baraza la Mawaziri la SADC ambao, katika mapendekezo yao 107 waliyoyawasilisha kwenye mkutano huo wa 39 wa wakuu wa nchi na serikali wa jumuiya hiyo kwa uamuzi, Kiswahili kilikuwa ni mojawapo.
Bofya hapa kusoma taarifa rasmi ya Ikulu: Taarifa ya SADC.pdf
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya na Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC) akiongoza kikao cha ndani cha Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya hiyo. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya Dkt. Taxs.
Chanzo: Mitandao na tovuti ya habarileo.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.