Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MRADI wa ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe unatarajia kuhudumia wakazi 30,024 kwa kuwapatia huduma bora za afya na kuboresha maisha yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 katika kituo hicho cha afya kilichopo Kata ya Chang’ombe jijini hapa.
Dkt. Method alisema “mradi huu utakapokamilika utasaidia wakazi wa Kata ya Chang’ombe kupata huduma za afya kwa ukaribu na kuboresha afya za wakazi wa kata hii. Jumla ya wakazi 30,024 watapata huduma bora za afya ambapo awali eneo hili lilikuwa halina kituo cha serikali kwa ajili ya kutoa huduma afya”.
Alisema kuwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe ulianza tarehe 24/12/2021 kwa fedha za tozo kutoka Serikali Kuu. “Mradi huu umepokea fedha kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ulipokea shilingi 250,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), Maabara na kichomea taka. Awamu ya pili mradi ulipokea shilingi 250,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa jengo pacha la mama na mtoto na upasuaji, kujenga jengo la kufulia na kujenga njia za kuunganisha majengo hayo (walkways). Pia Halmashauri ya Jiji imetoa shilingi 103,272,633.00 kwa ajili ya samani na vifaa tiba kupitia mapato ya ndani” alisema Dkt. Method.
Akihusianisha mradi huo na ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2022, alisema mradi una uhusiano wa moja kwa moja. “Mradi huu unauhusiano na ujumbe wa Mwenge wa Mwaka 2022 unaosema Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo; Shiriki kuhesabiwa tuyafikie maendeleo ya Taifa. Hivyo, basi zoezi la Sensa litasaidia kujua idadi ya sasa ya wakazi wa maeneo yatakayohudumiwa na kituo hiki ili kuwezesha kupanga mahitaji sahihi ya wananchi ikiwemo mahitaji ya dawa na vifaa tiba. Kwa sasa mradi huu utakapokamilika utatoa huduma kwa wakazi wapatao 30,024 wa Kata ya Chang’ombe na maeneo ya jirani” alisema Dkt. Method.
Kuhusu malengo ya mradi, alisema kuwa mradi umelenga kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa jamii. Mradi unalenga kuwapunguzia akina mama wajawazito umbali mrefu wa kupata huduma za kujifungua. “Malengo mengine kusogeza huduma za kliniki ya watoto chini ya miaka mitano na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua, pamoja na kutoa huduma za upasuaji, aliongeza.
Kwa upande wa mwananchi, Zuhura Nia alisema kuwa kituo hicho kitakapokamilika ni msaada mkubwa kwao. Wanufaika wakubwa wa kituo hicho ni kina mama na Watoto ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe unafanywa na mafundi wa ndani (Local fundi) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe na kusimamiwa na Wataalam kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.