Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Kituo cha Afya Chang’ombe kuhudumia wakazi 25,415 wa Kata hiyo kitakapokamilika na kuwaondolea wananchi usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya kituo cha Afya Makole jijini Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira alipokuwa akiongelea hatua za mwisho za ujenzi wa kituo hicho cha afya cha aina yake kinachojengwa katika Mtaa wa Msamaria, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Diwani Fundikira alisema “mpaka sasa hatua ya ujenzi imefikia asilimia 98 na ujenzi umeenda vizuri kwa kuwa wataalam wa ujenzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamekua wakikagua maendeleo ya ujenzi katika kituo hicho. Nimshukuru Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta wataalam kwa ajili ya kukagua kituo hiki ili kiwe katika hali bora na usimamizi mzuri”.
Alisema kuwa kutokana na ukubwa wa kituo hicho, kinatarajia kuhudumia kata nne za jirani. “Kituo cha Afya Chang’ombe kinaweza kuhudumia wananchi wapatao 25,415 hii ni kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi iliyofanyika Mwaka 2012, lakini pia kituo hiki kinatarajia kupokea wananchi wengine kutoka maeneo ya jirani kama vile Kata ya Mnadani, Miyuji, Chamwino, Nkuhungu na Kata nyinginezo ambazo hazina kituo kikubwa cha Afya. Hivyo, basi kituo hicho kitapunguza msongamano wa watu kwenye vituo vingine vya Afya na hata Hospitali ya Mkoa almaarufu General” alisema Diwani Fundikira.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Dalia Kapinga aliwataka wakazi wa kata hiyo kukilinda na kukitunza kituo hicho ili kiweze kuwahudumia watu wengi zaidi. “Gharama zilizotumika katika ujenzi wa kituo hiki ni kubwa, hivyo natoa wito kwa wananchi kukilinda na kukitunza ili kiweze kudumu na kuhudumia watu wengi na kwa muda mrefu” alisema Kapinga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Msamaria, Mwanaisha Matimbwa alisema kuwa wananchi wake walikuwa wakilazimika kufuata huduma za afya katika Kituo cha Afya Makole kilichopo mbali. “Hivyo, kupelekea shida pindi inapotokea kuna mgonjwa anahitaji huduma ya haraka na ukizingatia kituo cha Afya hakuna katika eneo la Chang'ombe” alisema Matibwa.
Ikumbukwe kuwa serikali kuu ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 250 fedha za tozo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho katika Mtaa wa Msamaria zilizojenga jengo la wagonjwa wa nje na maabara na kufikisha idadi ya vituo vya afya vya serikali kuwa vitano katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.